Na Raya Hamad (OMKR)
Imeelezwa kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inapanga mikakati na mipango ya maendeleo kwa kufuata Dira ya 2020 inayoendana na Mkakati wa kukuza uchumi na kuondosha umasikini Zanzibar na kulipa umuhimu suala la mazingira na uchumi nchi.
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bi Amina Khamis Shaaban kwenye ufunguzi wa Warsha juu ya kuendeleza mipango endelevu katika masuala ya mazingira na uchumi inayowashirikisha Wakurugenzi Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Hoteli ya Ocean View.
Bi Amina amesema lengo la kutoa mafunzo kwa wakurugenzi hao ni kuona mipango yote ya miradi ya maendeleo inafanikiwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa “kwa vile wakurugenzi mipango ndio mnaopanga mipango endelevu katika Wizara ni lazima mhakikishe kuwa masuala ya mazingira na uchumi mnayaingiza katika utaratibu wenu wa kazi kama tulivyokubaliana katika mpango mzima wa MKUZA “
Aidha Katibu Mtendaji huyo amesema ili nchi iweze kuwa na uchumi endelevu ni lazima kutunza na kulinda rasilimali muhimu ambazo ni chache kwa kuzingatia kuwa Nchi za visiwa kama Zanzibar ziko katika hali ambayo ni rahisi kuathirika likiwemo lile mabadiliko ya tabia ya nchi .
Nae Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr Islam Seif Salum amesema kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zilizomo ndani ya bahari hindi na hivyo kubahatika kupata mradi huu unaozishirikisha nchi za Seychelles, Comoro, Mauritius, Reunion na Madagascar,
Dk Islam amesema kuwa lengo la kuja kwa mradi huu ni kuweza kuzitunza mali asili chache kwa maendeleo ya nchi ikiwemo kuhifadhi na kuyalinda matumbawe, kuweza kukabiliana na majanga ya kimaumbile kama mafuriko pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kupanga mikakati endelevu.
Warsha hiyo ya siku tatu imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kufadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya pamoja na Kamisheni ya Bahari ya Hindi yenye makao makuu yake Mauritius .
No comments:
Post a Comment