Habari za Punde

SMZ Kuifanyia Kazi ya Ripoti Kamati Teule

Na Mwantanga Ame

HATIMAYE serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa itaipitia ripoti ya kamati teule ya Baraza la Wawakilishi na kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo, iliyoibua ukiukwaji wa sheria na matumizi mabaya ya madaraka katika taasisi kadhaa umma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar, alipokuwa akichangia ripoti hiyo.

Waziri Aboud alisema serikali inakubaliana na maoni na michango ya wajumbe wa Baraza hilo juu ya madai yaliyotolewa na kwamba itayafanyia kazi na hatimaye kutoa maamuzi sahihi.

Alifahamisha kuwa serikali itafanya uadilifu bila ya kumuonea mtu wakati wa kuchukua maamuzi hasa dhidi ya tuhuma za ubadhirifu na rushwa na kwamba mambo hayo yataendelea kupigwa vita na serikali.

Waziri huyo alisema dhamira ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona watendaji wake wanakuwa na maadili na heshima hali ambayo itawezesha kuwapatia huduma bora wananchi.

“Taarifa hii ninaiunga mkono kwani dhamira ni kukomesha tatizo la wizi wa mali za serikali, kwani Rais wakati akizindua Baraza alisema kuwa ataheshimu viongozi ili wawajibike kwa wananchi”, alisema waziri huyo.

Alisema Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akizindua Baraza hilo katika hotuba yake alivikataa vitendo vya rushwa kwani ni moja ya mambo yanayoharibu maadili ya nchi na kuhakikisha atapambana nalo.

Alisema katika hadi yake hiyo Dk. Shein, alieleza wazi kuwa katika kipindi cha miaka mitano atayoiongoza Zanzibar atahakikisha anaendeleza utawala bora wenye kuheshimu sheria.

Kuhusu malalamiko ya watendaji kutoshiriki katika vikao, waziri Aboud alisema agizo limeshatolewa kuwataka kushiriki vikao vya kamati na lazima waheshimu Baraza kwani serikali wanayoitumikia ndio msingi wa kutoa haki kwa wananchi.

Awali wajumbe wa Baraza hilo walipokuwa wakijadili ripoti hiyo ambapo kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma alisema serikali inapaswa kuwa makini kwani upo uwezekano wa taasisi kadhaa za serikali kuundiwa kamati teule za Baraza

Mwakilishi wa Magomeni Salmin Awadh, akichangia ripoti hiyo, alisema kwa vile bado aliyepewa kiwanja hicho hajakifanyia jambo lolote na wala kukilipia serikali ione haja ya kukichukua ili kirudi mikononi mwa serikali.

Alisema kinachoonekana watendaji wa serikali wameamua kwa makusudi kufanya udanganyifu unaojionesha kujitokeza katika maeneo mbali mbali ya utumishi wa umma jambo ambalo inahitaji kuona serikali inalisimamia ipasavyo.

“CCM haikubaliani na vitendo vya rushwa anaefanya hivyo ni kinyume na CCM na CCM haiko tayari kubeba misalaba ya wanaoenda kinyume na ahadi za CCM lazima waisimamie vizuri ili iende katika misingi inayotakiwa”, alisema Mwakilishi huyo.

Naye Hija Hassan Hija, Mwakilishi wa Kiwani, akitoa alisema kamati yao iliifanya kazi hiyo kwa umakini ikiwa ni hatua ya kuweza kujiridhisha kupitia vielelezo tofauti bila ya kujali itikadi zao kisiasa.

Mwakilishi wa nafasi za Wanawake, Asha Bakari Makame alisema Rais wa Zanzibar haiwezekani watendaji wa serikali kuendelea kuachwa kuifanya Ikulu ni sehemu ya biashara bali wanatakiwa kuitumia kwa kuwajibika zaidi.

“Sitakuwa tayari kuona CCM, inatiwa doa na watu kama siasa tumeshacheza zamani sasa basi ripoti hii apelekewe Dk. Shein, maana sisi kuna mambo hatuna Mamlaka nayo”, alisema Mwakilishi huyo.




1 comment:

  1. Hii ni ishara njema. Tusubiri Rais ayafanyie kazi mapendekezo ya Tume Teule. Kwa kweli ikiwa atafanya basi rushwa Zanzibar inaweza kupunguwa sana, kwa sababu hivi sasa watu wanakula na kutowa rushwa with impunity bila ya kujali vyombo vya usalama wala vya sheria. Kama mapendekezo yatafatwa basi Zanzibar itapiga hatuwa mbele. Hili lisimalizie hapa tu lakini uchunguzi ufanywe kwa wafanya kazi wote wa serikali waliojilimbikizia mali ambao wanajuilikana.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.