Habari za Punde

Wawakilishi Watakiwa Kuwa Walimu wa UKIMWI Majimboni

Na Salum Vuai, Maelezo

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wameagizwa kutumia nafasi na uwezo walionao kufikisha elimu ya kupambana na UKIMWI katika majimbo yao ili kupunguza kasi ya maambukizo mapya.

Agizo hilo limetolewa jana wakati wa warsha ya siku moja ya kuzijengea uwezo kamati za baraza hilo katika mikakati ya kutokomeza maradhi ya UKIMWI hapa nchini, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Bahari, hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Akifungua warsha hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej alisema wawakilishi wana majukumu makubwa katika kuhakikisha vita hivyo vinafanikiwa, hasa kwa vile wanasikilizwa na jamii katika majimbo wanayoyaongoza.

Wakiwa ni waangaliaji wakubwa wa shughuli za serikali, Ferej alieleza kuwa, wajumbe hao wanaweza kuhakikisha misimamo ya serikali juu ya masuala ya UKIMWI inaheshimiwa.

Aidha alisema, kutokana na nafasi yao katika kutoa maamuzi na kusikilizwa na jamii, wawakilishi hao wanaweza kunyanyua hadhi za watu wanaoishi na VVU katika majimbo yao, kushajiisha mijadala, kuhamasisha desturi, kuondosha imani potofu, itikadi za kisiasa na mila za hatari ili kuweka mazingira mazuri kwa kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Alieleza kuwa, UKIMWI bado ni tatizo la kitaifa na kimataifa, ingawa katika miaka kumi iliyopita, juhudi zimeonesha kuwa yapo mafanikio yaliyopatikana katika kujikinga na kupambana na ugonjwa huo usiokuwa na dawa wala kinga.

Waziri Ferej alitoa shukurani za dhati kwa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuwezesha kufanyika kwa warsha hiyo, pamoja na ushirikiano wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) katika kusaidia kuvishinda vita dhidi ya UKIMWI.

Akitoa mada katika warsha hiyo, muwezeshaji kutoka ofisi za UNDP/USAID Dk. Elly Ndyetabura, alisema uwajibikaji ni muhimu katika mwitikio wa UKIMWI duniani kwa sababu serikali, wafadhili na wadau wengine wamekuwa wakishindwa kutekeleza ahadi zao za kuongeza kiwango cha nyenzo na utoaji wa huduma.

Alisema katika miaka ya karibuni, wahisani na jumuiya za kimataifa zinazotoa misaada ya fedha kwa ajili ya kupambana na maradhi hayo, zimeeleza wazi kuchoka kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani, na kwa sasa zimekuwa zikipunguza bajeti inayotengwa kwa ajili hiyo.

Hivyo, alishauri hatua za baadae, zijikite katika kutafuta utaratibu wa kuongeza rasilimali za ndani utakaojumuisha wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi.

Pendekezo jengine, alisema, ni kuanzisha kamati za wataalamu chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itakayojumuisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wadau wa kitaifa na kimataifa.

Njia nyengine, alisema ni kamati za Baraza la Wawakilishi kuongeza usimamizi wa uwajibikaji katika utekelezaji wa masuala ya UKIMWI wa sekta za umma, pamoja na vyombo husika kuimarisha utaratibu wa kusimamia uwajibikaji wa Asasi za Kiraia na sekta binafsi.

Naye mtoa mada kutoka Tume ya UKIMWI Zanzibar Halima A. Mohammed, alisema katika vita hivyo, sekta za serikali zinapaswa kupanga mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kwani nazo zinaweza kuwa sababu ya kuongezeka kwa maambukizo mapya, hata pale zinapopanga kumaliza umasikini.

Akitoa mfano, alisema wizara zote zinaweza kuwa na nia nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi, lakini maisha yao yanapobadilika na kuwa na fedha nyingi, huweza kupata vishawishi vya kujitumbukiza kwenye starehe zinazoweza kuwa sababu ya wao kuambukizwa UKIMWI.

Wakichangia katika warsha hiyo, baadhi ya wawakilishi walishauri baraza hilo liondokane na mfumo wa sasa kuwa Idara ya Serikali na badala yake liwe taasisi inayojitegemea ili liweze kuwa na nguvu zaidi ya kufanya maamuzi katika vita dhidi ya UKIMWI pamoja na kupata fursa za kutafuta misaada ya kusimamia mapambano hayo.

Aidha, walisema maambukizo ya ugonjwa huo, yanasababishwa na Wazanzibari kusahau maadili na tamaduni zao, na kukumbatia wigo wa kigeni ambao hauna manufaa yoyote kwa jamii, na kutaka Serikali iweke mikakati maalumu ya kuhimiza familia ziongeze jitihada za kuchunga vizazi vyao kama walivyolelewa wao.

Akifunga warsha hiyo, Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, aliwataka wajumbe hao kuhakikisha wanayafanyia kazi kwa kuyafikisha katika jamii yale yote waliyojifunza ili mapambano hayo yaweze kuleta tija.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.