Habari za Punde

Waziri Mbarouk Aanza Kumwaga Cheche - Ataka Mabadiliko na Uwazi Sekta ya Michezo

Na Abdi Shamnah

WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk amewataka viongozi wa Baraza la Taifa la Michezo (BTMZ)na wale wa ZFA kubadilika na kufanya mambo kwa uwazi, hususan katika masuala ya fedha ili kufikia dhana ya usimamizi na uendelezaji bora wa soka la Zanzibar.

Amesema akiwa Waziri wa Wizara hiyo hatakubali kudanganywa na kiongozi yeyote na yule atakaemdanganya kwa makusudi, atamchukulia kuwa amemdharau, jambo ambalo hatalivumilia.


Waziri Mbarouk ametoa changamoto hiyo jana ofisini kwake Mnazi mmoja wakati alipokutana na viongozi wa BMTZ na ZFA, ikiwa ni kikao chake cha kwanza tangu ateuliwe kushika Wizara hiyo, kufatia mabadiliko yaliofanywa na Rais wa Zanzibar, hivi karibuni.

Alisema wakati umefika kwa viongozi hao kuondokana na ‘ukale’ wa kufanya mambo kwa kificho, hatua aliyosema imechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa migogoro na malumbano katioka Baraza na Chama hicho, na kudumaza ustawi wa soka.

Alisema hali ya maendeleo ya soka hivi sasa ni ya kusikitisha, ambapo Taifa limeendelea kupokea matokeo mabovu kutokana na michezo mbali mbali ya Kimataifa,inayotokana na misuguano isiokwisha kati ya viongozi na viongozi.

Waziri alisema ni jambo la kusikitisha kuwa hata baada ya miezi mitano kupita tangu Rais Shein alipoonyesha masikitiko yake juu ya mwenendo mbaya wa ZFA, lakini hadi leo hakuna mabadiliko yoyote yaliofanyika.

Alisema hali hiyo haiwezi kuachwa kuendelea, kwa kujua kuwa Zanzibar imebarikiwa kuwa na vijana wengi wenye vipaji vya soka, sambamba na kuwepo sera na sheria nzuri za kusimamia michezo.

Alisema akiwa kiongozi mkuu wa Wizara, atasimama kidete kuhakikisha ifikapo Novemba,2012 (pale Rais atakapotimiza miaka miwili tangu kuingia madarakani), hakuna tena simanzi juu ya mwenendo mbaya wa ZFA.

Katika kutilia mkazo msimamo wake, Waziri huyo alisema hatazamii kutumia nguvu katika kutoa maamuzi, lakini alionya kutumia kanuni, sheria na katiba ziliopo kama ufumbuzi wa mwisho kwa matatizo yatakayokosa suluhisho.

Katika hatua nyingine Waziri Mbarouk aliwataka viongozi wa ZFA kujenga mashirikiano na viongozi wa BMTZ na wale wa Wizara yake kwa kuamini kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia michezo yote nchini.

Aidha aliwataka viongozi hao kuelewa udhaifu mkubwa walionao kiutendaji, kiasi cha kushindwa kuandaa michuano ya Mapinduzi Cup na badala yake kuilazimu Wizara kuinusuru michuano hiyo kwa kuunda Kamati iliofanikisha vyema michuano hiyo.

Alisema pale viongozi wa Chama hicho watakapojipanga vyema na viongozi wa Wizara kuridhika na juhudi wanazofanya, hakutakuwepo kikwazo kwao cha kuwazuia kuandaa michuano yoyote ile, ikiwemo hiyo ya Mapinduzi Cup.

Vile vile Waziri Mbarouk aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa kutekeleza maagizo ya viongozi wakuu wa, ikiwemo agizo la Makamu wa kwanza wa Rais, Malim Seif aliloagiza kufanyika kwa marekebisho ya Katiba ya Chama hicho.

Wakitoa maelezo yao, viongozi hao walikiri kuwa soka la Zanzibar limeharibika kutokanana migogoro na udhaifu wa viongozi katika maeneo yote, ikiwemo Wizara,BTMZ na ZFA.

Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho, Al Haji Ameir, alimhakikishia Waziri huyo kuwa Chama chake kimepiga mstari wa kufuta ‘uozo’ unaoikabili ZFA na kuanza kazi ya kuendeleza soka kuambatana na miongozo iliopo, huku akieleza kuwa wako tayari kukosolewa na kuwakosoa wale wote wanaopotosha muelekeo wa soka la Zanzibar.

‘’Kinacholeta taabu kwa ZFA, ni viongozi wake kupenda kusema sana hatua inayowapa nafasi waandishi wa habari kuleta mkanganyiko wa mambo’, alisema Ali Mohammed, Makamo wa Rais wa ZFA Pemba.

Aidha Msaidizi Katibu wa ZFA Masoud Attai, alisema katika kuendeleza soka la Zanzibar, ZFA na BTMZ hufika wakati wakawa na mapatano na kufanya kazi kwa pamoja, lakini alisisitiza kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu umoja huo na kumuomba Waziri kuwa mkali dhidi ya 
waandishi wa aina hiyo.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Ali Saleh Mwinyikai aliwataka viongozi wa ZFA kupitia daraja za uongozi zilizopo kwa kuanzia na BTMZ kila pale watakapokuwa na matatizo badala ya kuchupa moja kwa moja kwenda kwa Wiziri, sambamba na kuwataka kutilia mkazo mashirikiano na ushirikishwaji wa wadau wote katika kuendeleza soka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.