Na Abdi Shamnah
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) inatarajiwa kupata ruzuku ya Ving’amuzi (decorders) laki mbili kwa ajili ya kuendeshea matangazo yake kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya watu wa China.
Msaada huo mkubwa unakaodiriwa kuwa thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 10 unalenga kuliwezesha Shirika hilo kupokea ving’amuzi hivyo, ikiwa ni hatua ya Serikali ya watu wa China kuisaidia Zanzibar katika
mchakato wake wa mageuzi kutoka mfumo wa sasa wa Analogia kuelekea ule wa Digital.
Hayo yameelezwa na Balozi mdogo wa China nchini Tanzania Chen Yimon, wakati alipokua na mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, ofisini Mnazi mmoja.
Kauli ya Balozi Chen inafuatia maombi mbali mbali yaliotolewa na Waziri Mbarouk, likiwemo lile la kuiomba nchi hiyo kuisaidia Zanzibar katika juhudi zake na kufikia mageuzi kamili kutoka mfumo wa teknolojia wa Analojia kuelekea Digitali.
Balozi Chen alisema China ikiwa mshirika na rafiki mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar, inatarajia kutoa msaada huo, ikiwa ni hatua za kuunga mkono juhudi za Zanzibar kufanikisha mageuzi hayo pamoja na kuziwezesha familia za Wazanzibari kupata mawasiliano mazuri kupitia mfumo wa Digitali.
Alisema mbali na msaada huo, pia ana matumaini makubwa kuwa Zanzibar itafanikiwa kupata mkopo wa Dola 28.5 kupitia kampuni ya HUAEI kama ilivyoomba ili kuharakisha mageuzi hayo, ambapo muda wa mwisho uliowekwa ni Disemba, 31, mwaka huu.
Aidha Balozi Chen alimhakikishia Waziri Mbarouk kuwa atalichukulia kwa uzito unaostahili ombi la kupatiwa mtambo wa kuchapishia kwa ajili ya gazeti la Serikali la Zanzibar Leo, sambamba na kuahidi kuutembele
Uwanja wa Mao tse Tung ulioelezwa unahitaji matengenezo kutokana na kuwa katika hali mbaya.
Akizungumzia suala la mafunzo kwa waandishi wa habari na watangazaji, Balozi Chen alimueleza Waziri Mbarouk, kuwa nchi yake mbali na kutoa fursa kadhaa za masomo ya juu na mafunzo ya muda mfupi kwa wanahabari wa Zanzibar, itaangalia uwezekano wa kuwa na program endelevu ya mafunzo kwa wanahabari.
Mapema Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk, aliiomba China kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati yake na Zanzibar na kuipongeza nchi hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Zanzibar, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Aliomba nchi hiyo kuendelea kuisaidia Zanzibar katika malengo yake ya kupanua wigo wa wataalamu katika sekta ya habari kwa kuweka program maalum ya mafunzo kwa waandishi na watangazaji.
Aidha aliomba kuangalia uwezekano wa kuufanyia matengenezo uwanja wa Mao tse Tdung, ambao alisema mbali na kubeba jina la mwasisi wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya China, lakini hali ilivyo sasa katika uwanja huo haulingani kabisa na sifa za kiongozi huyo.
Vile vile alimueleza balozi huyo kuwa hatua ya gazeti la Serikali (Zanzibar leo) kuchapisha makala zake nje ya Zanzibar, ni kasoro kubwa, hivyo kuomba nchi hiyo kusaidia upatikanaji wa mtambo ijapokuwa mdogo kwa ajili ya machapisho yake ya kila siku.
Kuna miradi kadhaa ya kimaendeleao katika sekta mbali mbali nchini, ambapo Jamuhuri ya watu wa China, iliisaidia Zanzibar, ikiwemo ujenzi/ukarabati wa Uwanja wa Amaan, mitambo ya kurushia matangazo ya Redio Dole, kiwanda cha Sukari na Manukato Mahonda na mingie mingi
No comments:
Post a Comment