Habari za Punde

Dk Shein Aendelea na Ziara Mkoa wa Kaskazini Pemba


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kutoka kwa Katibu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Afani Othman Maalim, alipotembelea Bonde la Ukele, kukagua Tuta la kuzuia Maji Chumvi, katika Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba, akiwa katika ziara ya kuangalia maendeleo ya jamii katika Wilaya hiyo leo.[Picha na Ramadhan Othman,Pemba.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imechukuwa juhudi ya kuwajengea Tuta la kuzuiya Maji ya Chumvi yasiingie katika Mashamba ya wakulima wa bonde la Ukele, Micheweni Pemba baada ya kuona juhudi za Kilimo zinazofanywa na Wananchi hao kuhusiana na Kilimo haziwafaidishi baada ya mashamba yao kuingia maji ya Chumvi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Ali Moh’d Shein, aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi na wakulima wa bonde la mpunga la Ukele mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Tuta la kuzuia maji ya chumvi kuigia katika bonde la mpunga na kueleza kuwa hali hiyo ilikuwa inamsikitisha sana na Serikali anayoiongoza ikaona haja ya kuwasaidia iliwaondokane na tatizo hilo.


Dk. Shein akiwa katika ziara yake anayoifanya ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ya kuangalia Shughuli mbali mbali za maendeleo aliendelea kusema kuwa Kilimo kinaweza kuwakombowa Wananchi na kuahidi serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Alisema kuwa Serikali imesikia Kilio cha Wakulima na itahakikisha kuwa inarahisisha matatizo ya Wananchi ikiwemo kuwapatia mbinu mbali mbali za Kilimo kwa kuwapatia Pembejeo na Wataalamu wa Kilimo.

Hata hivyo, Rais wa Zanzibar, aliwataka Wakulima na Wananchi kwa Ujumla kuhifadhi Mazingira kwa kupanda miti ikiwemo Mikandaa na kuilinda na wasiwaruhusu watu wengine kuikata kwani moja ya sababu ya kuingia maji katika Mashamba yao ni kukata Miti katika eneo hilo.

Aidha Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar, Affan Othman Juma, alieleza kuwa uhamasishaji wa Kilimo katika msimu huu ni mkubwa na kwa maana hiyo Wizara ilivuka Lengo la kulima kutoka ekari 2200 ya lengo hadi ekari 4527 sambamba kumalizika kwa pembejeo zote za Kilimo walizoagizia ambapo kwa sasa tayari wameshachukuwa juhudi ya kuagizia pembejeo nyengine.

Alisema kuwa baada ya kufika pembejeo hizo itawafikishia wakulima hao na wengine Kisiwani Pemba, iliwaweze kuzipata na kuzitumia katika msimu hu wa Kilimo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo, alieleza mikakati iliyowekwa ana serikali katika changamoto ya upandaji wa zao la mwani ikiwa ni pamoja na kuwapatia vifaa na kuongeza bei ya mwani.

Katika ziara hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Ali Moh’d Shein , alifika katika Kijiji cha Chimba kwa kuweka Jiwe la Msingi la kituo cha Afya ambacho kimejengwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe na Wafadhili mabali mbali.

Aliwapongeza Wananchi wa Shehia ya Chimba katika Wilaya ya Micheweni Pemba, kwa uamuzi wao walioufanya wa kujenga Kituo cha Afya katika Kijjiji hicho kwani suala la Afya ni jambo muhimu katika maisha ya mwanaadamu.

Alieleza kuwa Uamuzi wao wa kujijengea Kituo cha Afya katika kijiji hicho ni wa busara kwa Vile Ujenzi huo ulitokana na Fedha zao Mfukoni licha ya Umaskini walionao na kwamba suala la Afya halina ubaguzi wa aina yoyote.

Alisema kuwa kuwepo kwa Vituo vingi vya Afya katika Jimbo lao na Wilaya yao ni moja ya Faida ya Mapinduzi jambo ambalo kabla ya Mapinduzi halikuwepo katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

“ Ujenzi wa Kituo hicho ni moja ya maendeleo, kwa maana hiyo ni lazima waendelee kujiletea maendeleo katika Shehia yao” alisema Rais.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Ali Moh’d Shein, aliwataka Wananchi wasifikirie kubeza maendeleo kwani hayo ni masuala ya kila mmoja hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuchangia maendeleo.

“ Washajaisheni Wananchi wenzenu wa Chimba popote walipo iliwasaidie Maendeleo ya kijiji chenu, kwani huduma za Jamii hazina siasa na anae leta siasa anapotea” alieleza.

Aidha, aliwataka Wananchi wa Chimba kuwahimiza Watoto wao kusoma masomo ya Sayansi sambamba na kuwafuatilia maendeleo yao ili waweze kupata Wataalamu wa afya kutoka maeneo yao.

Dk, Shein, aliiagiza Wizara ya Afya kujiandaa kuwaleta Wataalamu wa afya katika eneo hilo kati ya hao wanao waandaa ili watoe huduma za afya katika Shehia hiyo ya Chimba.

Aliendelea kusema kuwa ataangalia uwezekano wa kifedha kupitia Wizara ya Fedha ,ilikuona ni namna gani watasaidia ili ifikapo Sherehe za Mapinduzi zinazo kuja kituo hicho kiweze kufunguliwa.

Kuhusu suala la ukosefu wa Skuli katika kijiji hicho aliiagiza Kamati ya Maendeleo ya Shehia hiyo kuanza Ujenzi wa Skuli itakayo wafanya Watoto wa maeneo hayo kupta huduma hiyo maeneo ya karibu na Serikali ipo itaangalia vipi isaidie.

Hivyo aliwataka Wananchi wa Chimba kuwa wastahamilivu na kuwaahidi kuwa Bara bara yao na kuahidi kuwa Serikali itaitengeneza kwa kiwango cha Kifusi ili iweze kupitika wakati wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.