Na Abdi Shamnah
UBALOZI wa China uliopo Zanzibar, unakusudia kuanzisha program maalum ya mafunzo, yenye lengo la kuwajengea uwezo wapishi katika hoteli za kitalii, kufahamu jinsi ya kusarifu mapishi ya mwani kwa ajili ya chakula cha binaadamu.
Hayo yametibitishwa na Balozi mdogo wa China aliopo Zanzibar Chen , katika kikao kilichowajumuisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii, Utamaduni na Michezo, Said Ali Mbarouk na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdillah Jihad Hassan, kilichofanyika katika ofisi za Ubalozi wa nchi hiyo Mazizini, ikiwa ni hafla maalum ya kuangalia jinsi zao hilo la mwani linavyoweza kusarifiwa katika mapishi tofauti.
Amesema hatua hiyo itawawezesha wapishi katika hoteli za kitalii nchini pamoja na wananchi kupika chakula hicho kwa umahiri na kuvutia wageni, sambamba an wananchi kutumia chakula hicho kwa ajili ya kuimarisha afya zao.
Alisema pale taaluma ya upishi itakaposambaa katika hoteli mbali mbali za kitalii, mbali na uzalishaji wa zao hilo kuongezeka, lakini pia wakulima wataondokana na tatizo la ukosefu wa soko unaowakabili hivi sasa.
“Tunalenga kuwafundisha Wazanzibari ili waweze kuutumia mwani kwa chakula, tunataka kuhakikisha zao hilo linapata soko kutoka kwa wenyeji na wageni, ikiwemo Wachina’, alisema.
Aidha alisema chakula cha mwani ni maarufu sana nchini China, ambapo hupatikana katika hoteli zote za kitalii na katika shughuli mbali mbali za kitaifa.
Chein alisema China inakusudia kupanua wigo katika shughuli za uvuvi visiwani humu pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwa na kituo cha utafiti kisiwani Pemba.
Aliwataka wananchi kufanya kazi kwa pamoja na kukuza shughuli za uvuvi, ili kuwawezesha kuinua viwango vyao vya maisha.
Mapema Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk alisema juhudi za Ubalozi wa China za kuhakikisha zao hilo linatumika nchini kwa ajili ya chakula, ni mapinduzi makubwa katika uchumi wa Zanzibar.
Alisema kwa muda mrefu sasa wakulima wa zao hilo wamekuwa wakilamikia ukosefu wa soko la uhakika na bei duni ya zao hilo, hatua inayokwaza maendeleo yao ya kiuchumi.
Alisema chakula hicho ni muhimu sana katika afya ya binaadamu, ikiaminika kuwa kinajenga siha na kutibu maradhi mbali mbali, ikiwemo Presha.
Nae Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdilah Jihad Hassan, alisema azma ya kuja kwa program hiyo ni faraja kubwa kwa Wazanzibari, kwa kuzingatia kuwa zao hilo limekuwa likizalishwa kwa wingi, huku likiwaacha wakulima wakililia soko.
Alisema kuja kwa program hiyo ndio ufumbuzi wa pekee utakaowahakikishia wakulima hao uwepo wa soko la ndani lenye kutosheleza mahitaji.
Katika tukio hilo ambapo pia lilihudhuriwa na wapishi wakuu wa Hoteli ya Bwawani, mpishi mkuu wa Ubalozi wa China Wang, alitoa mafunzo ya vitendo kwa viongozi hao jinsi ya kusarifu utengenezaji wa saladi “Sea weed salady’ pamoja na upishi wa keki ya mwani “sea weed cake”, ambapo wote walifurahia upishi huo.
No comments:
Post a Comment