Habari za Punde

Bodi ya chakula vipodozi ‘yaparura’. Yawaondosha watumishi watatu bandarini. Ni kwa kuruhusu tani 260 za mchele mbovu

Madina Issa na Mbarouk Abdalla

BODI ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar imewaondosha katika kituo cha kazi wafanyakazi watatu wa bodi hiyo waliopo Bandarini, wakihusishwa na tuhuma za utoaji wa makontena saba yenye mchele mbovu.

Wafanyakazi hao waliruhusu mchele huo tani 260, uingie katika soko kwa matumizi ya mwanadamu bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kuthibitisha ubora wake kwa matumizi ya mwanadamu.

Mrajis wa Bodi hiyo Dk. Burhan Othaman Simai, alisema hatua hiyo imekuja baada ya wafanyakazi hao kukiuka sheria na miongozo ya kazi ya Bodi hiyo kwa kuruhusumakontena hayo kwa kushirikiana na mfanyabishara Mohamed Hemed Mohamed.

Alisema bodi imechukua hatua ya kuwaondosha kufanyakazi katika sehemu hiyo ya Bandarini kama adhabu ya awali, huku wakiisubiri wizara ya Afya kutoa uamuzi dhidi ya wafanyakazi hao.

Alisema mchele huo aina ya Alminara unaotoka nchini Pakistan na uliingizwa nchini Mei 15 ya mwaka huu, ambapo tayari umeshasambazwa sokoni kwa matumizi ya binadamu.

“Wameruhusu makontena saba kati ya 10, ambapo baada ya kuchukuliwa sampuli ilimebainika kuwa mchele huo haufai kwa matumizi binadamu”,alisema Mrajis huyo.

Hata hivyo Bodi hiyo kwa kushirikina na Jeshi la Polisi tayari inaendelea na jitihada ya kuondosha mchele huo katika masoko mbali mbali na taratibu za kuangamiza au kuurejesha ulikotoka mchele huo zinafanyika kwa mujibu wa sheria.

Aliwataka watendaji wa Bodi yake kuwa waaminifu na kuachana na vitendo vya rushwa kwani hupelekea matatizo makubwa kwa afya za binadamu kwa kuwepo kwa bidhaa zisizofaa.

Kwa upande wa mmliki wa bidhaa hiyo Mohamed Hemed Mohammed alisema mchele wake ulipotoka nchini Pakistan ulikuwa mzima ambapo kampuni iliyosafirisha bidhaa hiyo MSC iliuweka mchele huo katika bandari ya Dar es Salam kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita na kusababisha kuharibika.

“Hii kampuni inawezekana ndio iliyosababisha hasara hii kukaa kipindi kirefu kwenye bandari ya Dar es Salam na ulipofika tu mchele huu hapa Zanzibar siku mbili tuliutoa lakini wataalam wa bodi baada ya kuchukua sampuli waligundua kuwa haufai”, alisema mfanyabiashara huyo.

Hivyo aliiomba serikali kumpa kibali ambacho kitamuwezesha kuirejesha bidhaa hiyo ilikotoka ili apate gharama zake na kuweza kufanyabiashara zake kama kawaida ambao mchele huo unagharimu zaidi milioni 290.

Mfanyabiashara huyo alikiri kuwa bidhaa hiyo kuwa ni mbovu na haifai kwa matumizi ya mwanadamu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina na bodi hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa wafanyakazi wa bodi hiyo kuhusishwa kwa utoaji wa bidhaa katika maeneo ya bandari bila ya kutoka kwa taarifa za mara kwa mara kama bidhaa hiyo inafaa au haifai kwa kula binadamu.


2 comments:

  1. Hya ni mambo ya ajabu hasa, Mimi nashangazwa sana na hii serikali yetu etu mtu kafanya uozo sehemu moja then anahamishiwa sehemu nyengine akarudie the same mistake mimi nnavoelewa mtu akifanya makosa ni kuhukumiwa sijawahi kusikia eti mtu anahamishwa sehemu nyengine.
    La pili nawatahadharisha watendaji wenye uchu wa rushwa haya ni makosa makubwa kwa mungu, atakuja kukuta mtu siku ya kiama anapewa kitabu chake ndani yake muna kesi za mauwaji ya watu kwa malaki aje kushangaa kumbe ni kwa sababu alikuwa na mamlaka akaruhusu bidhaa mbovu then watu wakauguwa cancer ikawa ndio sababu za vifo vyao. Tumuogope mungu na serikali hawa wafikishwe mahakamani ili iwe funzo kwa wengine wakiwemo wanaoruhusu madawa ya kulevya pale airport

    ReplyDelete
  2. Inasikitisha kuwaona Wafanyabiashara wakiwaangamiza wateja wao kwa kushirikiana na watendaji wasiowaadilifu na wenye tamaa iliopita mipaka. Aina hii ya wafanyabiashara walipaswa wafikishwe katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake, kwani wameshazoea kufanya uhalifu wakishirikiana na hawa madhalimu wenzao. Kwa kweli watendaji kama hawa walipaswa kusimamishwa kazi mara moja na pia ikibidi kuwapeleka mahakamani kwani licha ya kuwadhulumu ndugu zao pia wanaitia doa Serikali. Mh.Waziri husika pamoja na Serikali kwa ujumla tuache utaratibu wa kulindana kiasi cha kuweza kuwaenzi watumishi wasio na chembe ya huruma kwa wananchi wakiwemo watoto wetu ambao ni rahisi kuweza kuathirika na vyakula vya namna hii.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.