Habari za Punde

Wananchi waua majambazi Arusha


Joseph Ngilisho, ARUSHA
WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa na wananchi wenye hasira kwa kupigwa na vitu vizito baada ya kukutwa wakiwa katika harakati za kutaka kupora.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye alisema kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Ngusero sokoni jijini Arusha, ambapo watu hao walikuwa na gari aina ya Mark II yenye namba za usajili T 830 AHU.

Alifafanua kuwa, majambazi hao walionekana wakizunguka katika eneo hilo, ambapo wananchi hao waliwatilia mashaka na kuamua kuamshana kwa lengo la kuwazingira na kuwahoji.

Alisema kuwa, baada ya wananchi kuwazingira waliwapekua katika gari yao na kukuta wakiwa na vifaa mbalimbali vya kuvunjia milango ndipo walipowagundua sio watu wazuri na kuanza kuwashambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi ikiwemo mawe na rungu.

Andengenye aliwataja waliouawa kuwa ni Philipo Naftali (50), mwingine alitambulika kwa jina moja la Shida na mwingine ambaye hajafahamika jina lake hadi sasa hivi.

Hata hivyo jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi kwa ajili ya kuwasaka wale wote waliohusika na mauaji hayo kwani walikiuka sheria kwa kujichukulia sheria mkononi hali ambayo ni hatari sana kwani wangepaswa kuripoti tukio hilo polisi badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Alisema kuwa, jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi wa kuwasaka na wakishapatikana watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati huo huo, mkazi mmoja wa Longido aliyefahamika kwa jina la Abuu Hosea (22), alifariki dunia baada ya kusukumwa na kuanguka ghafla wakinywa pombe na rafiki.

Kamanda Andengenye alisema kuwa, tukio hilo limetokea mei 20 mwaka huu, majira ya saa 10:00 jioni katika eneo la Longido mjini katika bar ijulikanayo kama Zebra.

Alisema kuwa, siku ya tukio marehemu huyo alikuwa akinywa pombe na rafiki yake aitwaye James Mmasi (29) ambapo baadaye kulitokea ugomvi kati yao wawili baada ya Mmasi kumwambia marehemu kuwa waondoke ndipo walipoanza kubishana kati yao wawili hali iliyosababisha Mmasi kumsukuma marehemu na kuanguka chini.

Hata hivyo, marehemu huyo alikimbizwa katika hospitali kwa matibabu lakini mwishowe alifariki dunia wakati akiwa njiani, na mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi na pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.