Habari za Punde

Utendaji Mamlaka ya Usafiri Baharini Watiliwa Shaka

Na Hafsa Golo
MKURUGENZI wa kampuni ya Seagull, Said Abdulrahman amesema haoni umuhimu wa kuwepo Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (ZMA), kwani Mamlaka hiyo imeshindwa kujiamini katika utoaji wa maamuzi.

Mkurugenzi huyo alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ambapo alishangaa kwanini taasisi hiyo iliyopewa mmalaka ishindwe kusimamia vyema majukumu yake na kwa kujiamini.

Kauli ya mkurugenzi huyo wa kampuni ya usafiri baharini imekuja baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, kushindwa kumpata jawabu la uhakika kwanini meli yake Mv Seagull imezuiliwa.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa vyombo vya usafiri wa baharini Zanzibar vinapopata hitilafu ama kutilia shaka ya kuwa na hitilafu, lazima wachunguzi watoke Dar-es-salaam, na kuhoji nini maana ya kuwepo kwa Mamlaha hiyo visiwani hapa.

Alisema kinachoonekana ni kwamba ZMA, haina wataalamu katika uchunguzi wa hitilafu za meli ama waliopo hawajiamini, hali ambayo imekuwa ikisababisha shida wasafiri wa Zanzibar.

"Ni bora Mamlaka hii ivunjwe au ihamishiwe Dar es Salaam na iunganishwe na SUMATRA, kwa sababu uwepo wake hivi sasa hauonekani faida yake”, alisema.

Alifahamisha kuwa inasikitisha serikali kuwaajiri watu kwenye mamlaka hiyo huku wakipokea mishahara inayotokana na kodi za wananchi, ambapo wanashindwa kuwarejeshea huduma wananchi jambo ambalo hawawatendei haki.

Mbali na hayo alisema haoni sababu za msingi hasa za kusimamishwa kuendelea na safari zake kwa hitilafu iliyojitokeza kwenye boti ya Seagull ambayo ni ya kawaida kwa vyombo vinavyotumia mashine.

Alisema kuwa uongozi unashughulikia usafiri wa vyombo hivyo ni vyema vikazingatia sheria nataratibu zilizowekwa ili kuwepusha upendeleo kwa baadhi ya vyombo hivyo pale hitilafu zanapotokezea.

Akijibu tuhuma hizo, Naibu waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Ussi Gavu, alisema ZMA ina wajibu wa kuvikagua vyombo hivyo na wanatekeleza kazi zao ipasavyo tena kwa mujibu wa sheria zilizowekwa nchini.

Naibu huyo alisema wakaguzi wa meli waliopo katika Mamlaka hiyo wana ujuzi na wenye kuwajibika vyema katika kutekeleza majukumu yao.

Akizungumzia juu ya meli hizo kusubiri wachunguzi kutoka Dar es Salaam, Gavu alisema hivyo ni vitengo viwili tofauti lakini vina ushirikiano katika utendaji wa kazi zao na kueleza kuwa hakuna tatizo katika ushirikiano wa namna hiyo.

Gavu alisema suali la ukaguzi wa meli kwa safari za kila siku ni la Nahodha na Fundi mkuu, hivyo wajibu wa serikali kukagua vyombo hivyo kila baada ya miezi minne au ikiwa haikuridhika au ikijenga dhana ya kasoro za vyombo hivyo lazima izuwie.

Aidha aliwataka wananchi kuelewa kuwa matatizo yanayojitokeza katika vyombo hivyo na mara tu kuanza safari zake huwa mamlaka husika ishafuatilia tatizo hilo na limehakikisha lishafanyiwa marekebisho yanayostahili ndipo wanaporuhusiwa kuendelea na safari zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.