Habari za Punde

Kitengo cha Urithi Baharini ni Sehemu Muhimu ya Kuvutia Wageni


 Kamishna wa Utamaduni na Michezo Zanzibar Hamadi Bakari Mshindo akifafanua jambo katika kikao cha kujadili suala la uharibifu wa mambo ya bahari kilichofanyika leo ukumbi wa Makumbusho ya Kasri uliopo Forodhani mjini Zanzíbar kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Zanzibar Dkt.Amina Ameir



 Mkuu wa Kitengo cha Urithi wa Baharini Zanzibar Fakih Othman akielezea changamoto zinazokabili kitengo hicho katika kikao cha kujadili suala la uharibifu wa mambo ya baharini kilichofanyika leo ukumbi wa Makumbusho ya Kasri Forodhani mjini Zanzíbar
Mkuu wa Makumbusho ya Mnazi mmoja Zanzibar Ameir Ibarahim Mshenga akionesha picha ya Watafiti wa mambo ya bahari waliyofanya Zanzibar katika kikao cha kujadili suala la uharibifu wa mambo ya bahari kilichofanyika leo ukumbi wa Makumbusho ya Kasri uliopo Forodhani




Picha zote na Iddy Haji-Maelezo Zanzíbar


Na Faki Mjaka-Maelezo

Kamishna wa Utamaduni na Michezo Zanzibar Hamadi Bakari Mshindo amesema ipo haja ya Kitengo cha Urithi wa Baharini kuwa makini na jasiri katika kusimamia vyema urithi wa Zanzibar kwani kitengo hicho kinaweza kuwa sehemu muhimu ya kuvutia watalii ambao wanaweza kuzuru maeneo ya urithi huo.

Amesema maeneo ya Urithi wa Bahari ni sehemu muhimu kwani Wageni kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakiyatembelea ili kujua historia ya maeneo hayo jambo ambalo linaweza kuwa kichochoe kikubwa cha kuongeza wageni ambao huja kuitembelea Zanzibar kila msimu.

Kamishna Mshindo ameyasema hayo katika kikao cha kujadili suala la uharibifu wa mambo ya bahari kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Makumbusho ya Kasri uliopo Forodhani mjini Zanzíbar.

Amesema lengo la kikao hicho ni kujadili njia nzuri za kuhifadhi urithi wa baharini ambao kama utawekewa mikakati mizuri unaweza kuisaidia Zanzíbar kupiga hatua kwani ni eneo muhimu la kuvutia watalii.

Kamishana amesema kutokana na umuhimu wake kuna haja pia ya wadau walioshiriki katika kikao hicho kuwa na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha mazingira ya urithi huo yanahifadhiwa kwa ajili ya maslahi ya taifa.

Amefahamisha kuwa Urithi huo ni pamoja na Meli ambazo zilizama katika bahari, mapango na vitu ambavyo vimekuwa vikitupwa katika bahari mambo ambayo yanageuka kuwa urithi ambapo watu kutoka maeneo mbalimbali huwa na hamu ya kujua historia ya vitu hivyo.

Aidha urithi huo huchangia kuongezeka kwa mazalio ya viumbe hai wa bahari ambao hugeuza maeneo hayo kuwa nyumba zao za kujihifadhia na hivyo kusababisha ongezeko la samaki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Dkt.Amina Ameir amesema kuna haja ya jamii kuelimishwa juu ya umuhimu huo sambamba na kuacha tabia ya kuchukua mabaki ya urithi huo kwa lengo la kwenda kuuza mabaki hayo kwa watu wasio husika.

Amesema kuna Wazamiaji ambao hutumiwa na watu kwa lengo la kuzamua mabaki ya Meli na Mamboti ambayo yalizama na kwenda kuyafanya bishara ya chuma chakavu jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kisheria.

Ameongeza kuwa Idara yake itachukua mkakati wa makusudi kwa kushirikiana na wadau husika kuwafahamisha wananchi kuwa Mabaki ya meli zilizozama ni urithi wa Nchi na hivyo wananchi hawana haki ya kuchukua mabaki hayo bila kupata idhini ya Kitengo cha Urithi wa Mambo ya Bahari.

Akitoa historia yake Mkuu wa kitengo hicho Fakih Othman amesema kitengo hicho kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa na malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti juu ya urithi wa baharini katika maeneo yote ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Malengo mengine ni pamoja na kushirikiana na taasisi mbalimbali za nje na ndani ya nchi zinazojishughulisha na uhifadhi na utunzaji wa urithi wa Baharini.

Fakih ametaja changamoto zinazokikabili kitengo cha Urithi wa Mambo ya Baharini kuwa ni pamoja na uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi, ukosefu wa mafunzo pamoja na kutokuwepo kwa fungu maalum kwa ajili ya kuendeleza kitengo hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.