WIZARA ya Miundombinu na Mawasiliano imeeleza vipaumbele ulivyoviweka kuwa ni pamoja na kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, anga, bahari pamoja na uimarishaji wa mawasiliano.
Uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ulieleza hayo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.
Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar uliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ambao pia, ulihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Uongozi huo, ulieleza kuwa katika kufanikisha hayo, Wizara imejidhatiti kuimarisha usalama wa usafiri wa nchi kavu, bahari na anga.
Waziri wa Wizara hiyo Hamad Masoud, akisoma utangulizi wa taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo, alisema kuwa vipaumbele vinavyotekelezwa na Wizara vinaendana na utekelezaji wa malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZAII) ambayo pia yamezingatia Dira ya 2020`
Wizara hiyo pia, imeeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kiboje Mabonde ya mpunga tayari umeshakamilika.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa Wizara ilikaa na Wizara tatu na kukubaliana kuwa barabara inayopita katika ya msitu wa Ngezi ijengwe kwa njia ya kuchanganya udongo na chokaa au saraji huku kukiandaliwa mchakato wa kutengenezwa barabara ya kudumu sehemu zilimo pita umeme.
Uongozi huo pia, ulielezea Mpango Mkuu wa Usafiri Zanzibar kwa miradi ya Maendeleo wa sekta ya usafiri wa barabara na kuelezea barabara za Unguja na Pemba ambazo tayari zimeshakamilika zikiwemo za vijijini.
Pia, uongozi huo ulieleza Mpango huo Mkuu wa Usafiri kwa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na utayarishaji kwa barabara zinazoingia mjini ikiwemo Malindi-Mnazimmoja, Welezo-Amani Kariakoo, Bububu-Mtoni-Kinazini-Malindi, Bububu-Mahonda- Mkokotoni, Tunguu-Magomeni-Mkunazini na Mtoni Kiembesamaki.
Aidha, Wizara ilieleza kuwa ujenzi wa barabara za vijijini Kusini Pemba, Mtambile-Kengeja, Mtambile-Kangani, Mizingani-Wambaa, Kenya-Chambani, Chanjamjawiri-Tundauwa na Chanjani-Pujini tayari umekamilika.
Wizara hiyo pia, ilieleza mchakato unaondelea katika kuuwekea taa uwanja wa ndege wa kisiwani Pemba sanjari na kuliwekea mazingira mazuri jengo la kupumzikia abiria katika uwanja huo wa ndege wa Pemba.
Kuhusu matengenezo ya eneo lililodidimia katika Gati ya Mkoani, Uongozi huo ulieleza kuwa tayari matengenezo yake yameshakamilika huku matengenezo ya kiungo cha gati hiyo yanaendelea. Pia uongozi huo ulieleza kuwa kreni mbili za tani 70 na 20 zimenunuliwa katika uimarishaji wa Bandari ya Malindi.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alieleza kuwa kuweka matuta barabarani sio suluhisho la kupunguza ajali bali suluhisho kwa madereva ni kufuatwa kwa sheria za usalama barabarani zilizowekwa ili kuepuka ajali zisitokee.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kuwaandaa watu juu ya Mpango Mkuu huo wa ujenzi wa barabara hasa zile za Tunguu-Magomeni na Bububu-Mahonda-Mkokotoni, ili wananchi waliowekewa alama katika nyumba zao ziliopo pembezoni mwa barabara hizo wawe na uwelewa juu hatua hiyo na kinachofuata baadae.
Dk. Shein pia, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kuimarisha miundombinu na mawasiliano kwa upande wa Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment