BALOZI Mdogo wa India aliyepo Zanzibar, Pawan Kumar amesema nchi yake itahakikisha inatoa kila msaada kuiona Zanzibar inapiga hatua mbele kimaendeleo.
Balozi huyo alieleza hayo ofisini kwake Migombani mjini hapa, katika hafla fupi ya kuwakabidhi viza maofisa wawili waandamizi wa serikali ya Zanzibar ambao wamepatiwa nafasi za masomo ya muda mfupi nchini India.
Maofisa walipatiwa nafasi hizo za mafunzo ya wiki nne ni pamoja na Hassan Ali Mohamed kutoka Idara ya Mkurugenzi wa Mashitaka na Rashid Hadid Rashid ambaye anafanyakazi katoka ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Chake Chake.
Balozi Kumar alisema nafasi walizopatiwa maofisa hao ni kielelezo cha India katika kusaidia maendeleo ya Zanzibar kwani elimu watakayoipata itasaidia kuleta mabadiliko.
Alifahamisha kuwa India itaendelea kushirikiana na Zanzibar sambamba na kuhakikisha kila nafasi za masomo zinazotolewa na serikali ya nchi hiyo wanapatiwa pia maofisa wa Zanzibar.
“Nafasi hizi za mafunzo zimetolewa na kufadhiliwa na serikali ya India, chini ya mradi kiufundi wa ushirikiano wa kiuchumi (ITEC)”, alisema Balozi huyo.
Alisema nafasi hizo za masomo ni miongoni mwa nguzo ya kuongeza ushirikiano na kwamba elimu wanayopatiwa maofisa hao inalenga kuhakikisha maendeleo ya Zanzibar yanakua kwa haraka.
Kwa upande wake Hassan Ali Mohamed, alisema nafasi aliyoipata itamuwezesha kuongeza ujuzi katika utawala na kuhakikisha elimu atakayoipata nchini India itasaidia maendeleo ya Zanzibar.
Naye Rashid Hadid Rashid aliishukuru serikali ya India kwa msaada wake huo na kuiomba iendelee kutoa nafasi hizo kwa maofisa wa Zanzibar.
Mwaka uliopita chini ya parogramu ya ITEC, maofisa 48 kutoka Zanzibar walipata mafunzo ya fani mbali mbali nchini India.
No comments:
Post a Comment