Habari za Punde

Madrasah Ziende na Wakati - Maalim Seif

Na Hassan Hamad  OMKR

Wakati umefika kwa wazazi na walimu kuzibadilisha madrasa za Qur’an kuwa za kisasa na zinazokwenda na wakati. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo katika hafla ya maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Munira Madrasa and Islamic Propagation huko Magomeni Makuti mjini Dar es Salaam.

Amesema madrasa zikiwa na mazingira bora, watoto  watakuwa na ari ya kwenda kujifunza kwenye madrasa hizo na hatimaye kujenga jamii yenye maadili bora.Sambamba na hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais amesisitiza haja ya kuwekwa mkazo kwenye elimu ambayo itawasaidia vijana wanaohitimu kuwa na upeo mkubwa wa dini, pamoja na kujiweka katika mazingira mazuri kukabili ushindani wa ajira.

Aidha Maalim Seif ametoa wito kwa waislamu kuepukana na mambo ya kutengana na badala yake kuwa kitu kimoja kwa maendeleo ya dini na kwa ya  vizazi vijavyo.

Ameitaka jamii kubadilika na kuthamini elimu na malezi  yanayotolewa kwenye madrasa za Qur’an, na kuwasisitiza wazazi kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto katika jamii.

Akisoma risala ya Jumuiya, Katibu wa jumuiya hiyo ustadh Juma Rashid amesema madrasa hiyo ambayo inatoa elimu kwa rika zote kupitia njia mbali mbali, ina mpango wa kujenga skuli kubwa ya kiislamu katika eneo la Mlandizi itakayogharimu shilingi bilioni 3 nukta 6.

Amesema kwa sasa wanaendelea na juhudi za kutafuta umiliki wa eneo hilo la ekari kumi, na kuiomba serikali na taasisi binafsi kushirikiana na jumuiya hiyo ili iweze kutimiza malengo yake iliyojiwekea.

Kwa upande wake Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji amewataka walimu wa madrasa kuwa na subra na wasichoke kutoa elimu kwa vijana wa kiislamu, licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kipato kidogo, lakini wategemee malipo makubwa zaidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maulid hayo yamezishirikisha madrasa mbali mbali kutoka mikoa tofauti ya Tanzania ikiwemo Arusha na baadhi ya mikoa ya Zanzibar..

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.