Habari za Punde

Mtuhumiwa wa Kukinyofua Pua Kichanga Apandishwa Mahakamani

Na Omar Hassan, PEMBA

MTUHUMIWA wa Mauaji ya mtoto mchanga kwa kumnyofoa pua kwa mara ya mwanzo amefikishwa kataka mahakama ya Mwanzo ya Chake Chake kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mtuhumiwa huyo Mussa Bilali Mussa (73) mkaazi wa Mshangama Wesha Chake chake, Pemba alifikishwa mbele ya hakimu Mohamed Subeit Khamis wa Mahakama ya Mwanzo.

Akisomewa shitaka lake na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Albaghir Yakout Juma mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo alidai kuwa Mei 15 mwaka huu majira ya saa 4.50 asubuhi huko Mshangama Wesha katika wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba mtuhumiwa huyo alimuua Arafa Haji Silima mwenye umri wa mwezi mmoja na siku tatu.

Mwendesha Mashitaka huyo alisema kosa la hilo la kuua ni kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria namba 6 ya mwaka 2004, Sheria za Zanzibar.

Mtuhumiwa huyo hakutakiwa kujibu kitu chochote Mahakamani hapo kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka kisheria kusikiliza kesi yake na kwamba kesi hiyo inapaswa kusikilizwa Mahakama kuu.

Hata hivyo Mzee huyo aliiomba Mahakama hiyo impatie dhamana kutokana na kuwa umri wake ni mkubwa pia ana mwanawe wa kike ambaye ana mtoto mchanga wote wanamtegemea yeye kuwapatia huduma na hawana mtu mwengine wa kuwahudumia.

Pamoja na sababu hizo upande wa mashitaka ulisema hauwezi kumpatia dhamana mtuhumiwa huyo kutokana na kuwa kosa hilo la mauaji halina dhamana kisheria lakini pia Mahakama hiyo haina uwezo kisheria wa kufanya hivyo.

Mtuhumiwa huyo amepelekwa rumande hadi Mei 29 mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.