Habari za Punde

Polisi Wastaafu Wakosa Pencheni Miezi Mitano Sasa

Na Mwantanga Ame

WASTAAFU wa Jeshi la Polisi, wameulalamikia uongozi wa Jeshi hilo kwa kuwacheleweshea mafao yao katika kipindi cha miezi mitano hivi sasa jambo ambalo limewafanya kuwa katika hali mbaya kimaisha.

Wastaafu hao waliliambia gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao kuwa wanashindwa kufahamu ni kwanini wamecheleweshewa malipo yao jambo linalowafanya kuingia katika madeni madukani.

Walisema hivi sasa wamekuwa wakikumbwa na ukata mkubwa wa kuendesha maisha yao baada ya kuanza kuaminiwa na wanaowapa huduma katika maduka ya uraia kwa vile muda walioahidi kulipa madeni yao kupitiliza.

Walisema kikawaida Jeshi hilo limekuwa likiwalipa pencheni yao ndani ya kipindi cha miezi mitatu kutokana na makubaliano waliyoyafanya lakini jambo la kushangaza kuona hivi sasa muda huo hupita zaidi.

Wakitoa mfano walisema kwa mwaka huu walitarajia kupata fedha hizo mwezi Machi, lakini baada ya kufika muda huo waliambiwa hawatalipwa ili kusubiri kufanyiwa uhakiki ili kutambuliwa waliohai na waliofariki.

Walisema zoezi la uhakiki huo lilifanyika mwezi Aprili, kwa muda wa siku mbili tuu, lakini jambo la kushangaza kuona hadi mwezi huu unaingia hakuna kilichoingizwa mpaka sasa.

Wastaafu hao, walifahamisha jambo linalowashangaza kuona wanapojaribu kuwauliza viongozi wao wanawaeleza kuwa mambo yao tayari yameshafanyiwa kazi na kuwataka kwenda Benki kuangalia mafao yao.

Hata hivyo, walieleza wanapokwenda Benki hukuta kinyume na maelezo ya viongozi hao kwa kuelezwa na makarani wa Benki kuwa bado mambo yao hayajaingizwa.

Kutokana na hali hiyo wastaafu hao wameeleza wanapata ugumu wa kufahamu ukweli halisi wa suala hili na wameanza kuwa na wasiwasi juu ya wasimamizi wa mafao ya askari wastaafu.

« Walitwambia sababu ni usajili kutambua waliokufa na walio hai, tumekubali lakini zoezi hilo lilifanyika siku mbili tu likaisha kwa kutambua baada ya hapo tayari wangeshatambua na kutumalizia tuliohai lakini sivyo kabisa huu ni mwezi wa tano unaisha » Alisema Wastaafu hao.

Walisema hali hiyo imekuwa ikiwapa ugumu kuendesha maisha yao huku baadhi yao wakiwa wagonjwa ambao mara nyingi hutegemea fedha hizo waweze kujitibu.

Wastaafu hao waliutaka Uongozi wa Jeshi la Polisi kuliangalia suala hili kwa makini ikiwa ni hatua ya kuwatunza askari wake wasiwe ombo omba ama kufikishwa katika vyombo vya sheria kutokana na kuwa na madeni ambayo wangeweza kuyaepuka.

« Tunaomba viongozi wetu watusaidie kwa hili maana hivi sasa hali ni mbaya na bado sisi tunaimani kuwa tupo pamoja nao hata kama ni wastaafu tusionekane tukiwa nje na letu limeisha » walisema Wastaafu hao.

Hata hivyo wastaafu hao walikosoa utaratibu wa uhakiki kufanywa ndani ya mwezi uliokuwa wakitarajiwa kufanyika malipo yao kwani inaweza kuwa ndio chanzo cha kutokea tatizo hilo.

Walisema kwa vile Jeshi hilo lilitambua kuwa linahitaji kufanya uhakiki wafanyakazi wanaopokea pencheni, walipaswa kuifanya kazi hiyo ndani ya mienzi mitatu ambayo wao walikuwa wakisubiri kupata pencheni yao na sio baada ya muda huo kufika jambo ambalo linaweza kuchangia tatizo hilo.

« Walikuwa waje mapema katika ile miezi mitatu tunayosubiri kupata pencheni yetu sasa muda wetu utapofika kupata fedha zetu usichanganyike na mambo mengine hapa tutakuwa tunaenda vizuri tufikirie mienzi mitatu mtu anaishi kwa madeni kisha mwezi unaojua madeni ynayaondoa hupati kitu wanatutia presure » Walisema Wastaafu hao.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, akizungumzia na Zanzibar Leo alisema suala hilo halipo kwa vile tayari wameshalifanyia kazi kwa kuwalipa wafanyakazi wote wa Taasisi hiyo pamoja na wastaafu.

« Sio kweli kama kuna madeni hayo sisi tumeshawalipa mishahara na mafao askari wote hatuna madeni » Alisema Kamishna Mussa.

Ingawa Kamishna huyo kueleza kuwa mambo yako safi katika masuala ya pencheni hiyo lakini bado Wastaafu hao hadi jana mchana tulipozungumza nao tena walisema hilo halina ukweli kwani walienda Benki na kukuta hakuna kitu kilichoingizwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.