Habari za Punde

Rais Kikwete Azindua Tovuti ya CCM

Na Rajab Mkasaba

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Mrisho Kikwete amezindua tovuti rasmi na blog ya CCM na kueleza kuwa lengo ni kuifanya chama hicho kwenda na wakati uliopo.

Uzinduzi huo umefanyika katika uwanja wa ofisi ya CCM Makao Makuu Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama hicho pamoja na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya Juu, Sekondari, wawakilishi wa UVCCM wa Mkoa huo na wengineo.


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alihudhuria pamoja na viongozi wengine akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Amani Abeid Kaume, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Mhe. Pius Msekwa, Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama pamoja na viongozi wengine wa CCM. 

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa, alieleza kuwa wakati umebadilika na kutokana na teknolojia ya mawasiliano kukua chama hicho kimeona haja ya kwenda na wakati na kuingia katika teknolojia hiyo ya mawasiliano.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa kutokana na teknolojia hiyo kukua na huku cama hicho kikiwa na malengo za kuwafikishia habari na taarifa mbali mbali wanachama wake popote pale walipo ndio imeona njia hiyo itasaidia kufikia malengo hayo. 

Alisema kuwa dunia ya leo hasa vijana wanahitaji kutumia njia za habari za kisasa zikiwemo za kutumia tovuti na blog ambapo teknolojia hiyo inarahisisha mawasialiano kwa kiasi kikubwa hivyo uwamuzi huo wa CCM kupitia Idara yake ya Uenezi umechukua uwamuzi sahihi wa kuanzisha na kuimarisha mawasilaino hayo. 

 “Na sisi Chama Cha Mapinduzi uwamuzi wetu wa kuamua kwenda na wakati kwa kuanzisha tovuti na blog ni utaratibu mzuri ambao utawasaidia wananchi wa ndani na nje kupata taarifa za chama chao”,alisema Rais Kikwete. 

Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kutoa taarifa kwa watu wengi kwa muda mfupi na watu wengi wamekuwa wakitumia teknolojia hiyo kutokana na urahisi na unafuu wake. 

Rais Kikwete alisema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia hiyo mpya ambapo inasemekana hivi sasa watumiaji wa intaneti mwaka 2000 walikuwa ni laki 115,000 na mwaka jana watumiaji wamefikia milioni 4.9. 

Pia, alieleza kuwa nchini kuna blog zisizopungua 50 na watu milioni 3 kwa siku wanatumia blog hizo na asilimia 48 za watu ni wa hapa nchini huzitembelea. Alisema kuwa watumiaji wa facebook wamefikia 437040, kwa siku ni kutokana na urahisi na wepesi wa habari sanjari na kuwa huduma nyingi ni za bure na zina unafuu na CCM kuingia katika mfumo huo ni sahihi huku akisisitiza kuwa chama hicho ni chama cha vijana wanaopata misingi kutoka kwa wazee wa chama hicho hivyo ni lazima kiende na wakati. 

Sambamba na hayo, Rais Kikwete alisema kuwa tovuti hiyo itasaidia kutangaza mafanikio na changamoto za chama hicho na kutoa agizo kwa Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi Bwana Nape Nnauye katika kuhakikisha kuwa tovuti hiyo inadumu na inaendelea kuwa hai kutokana na mifano mbali mbali ya tovuti kadhaa nchini kutodumu. 

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alitoa shukurani kwa Katibu Mkuu wa CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM pamoja na wale wote waliosaidia kutayarisha blog na tovuti hiyo. 

Wakati huo huo, Rais Kikwete aliieleza hadhara hiyo pamoja na vijana waliohudhuria kuwa katika kikao cha leo, chama hicho kitaunda Mkoa wa CCM wa Vijana ambapo baada ya hapo taratibu nyengine za kuchagua viongozi zitafuata na kusisitiza kuwa Mwenyekiti na Katibu wa Mkoa huo watakuwa ni Wajumbe wa NEC. 

 Mapema Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi Mhe. Nape Nnauye alisema kuwa CCM tokea kuanzishwa imekuwa ikifanya mambo mengi na kina historia kubwa lakini kimekuwa kikikabiliwa na changamoto ya wanachama wake kutopata taarifa. 

Alisema kuwa ushahidi unaonesha kuwa jamii hasa vijana wanatumia sana teknolojia ya habari ya mawasialino kwa kiasi kikubwa katika maisha yao ya kila siku. 

Katibu Mwenezi huyo alisema kuwa tovuti na blogi hizo zitakuwa na taarifa nyingi za vijini ambako hivi sasa nako kumekuwa na mwamko mkubwa wa mawasialiano. Aidha, alisema kuwa tovuti hiyo itakuwa na sifa za pekee ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia ya ‘Content managing system” ambayo itaunganishwa na mitandao kadhaa ya kijamii.

Alisema kuwa njia hizo za mawasiliano zilizozinduliwa na Rais Kikwete zitatoa taarifa mbali mbali za chama na zitatumia lugha zote za kimataifa ikiwemo kiengereza, kiarabu, kichina na nyenginezo hatua ambayo itasaidia kutoa taarifa ndani ya nchi, katika nchi za Afrika na dunia nzima. 

Pamoja na hayo, Nape alisema kuwa chama hicho kimeangalia uwezekano wa wanachama kujiunga online na kuweza hata kujaza fomu zitakazohitajika na kuzituma baada ya kupata maelezo hatua hiyo pia, itasaidia pia kujaza fomu zikiwemo za wagombea wa nafasi mbali mbali za chama. 

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, iliyoketi mjini hapa chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete, pia, iliteua Makatibu wa chama hicho wa Wilaya 32 ambapo watapangiwa vituo vyao vya kazi hivi karibuni. 

Nae Katibu wa CCM, Mkoa wa Dodoma Mhe. Willium Kusila akitoa neno la shukurani alieleza kuwa hatua hiyo ya CCM itaweza kuimarisha mawasialino na kuweza kuwapelekea taarifa wanachama wa CCM kwa muda mfupi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.