Rais wa Zanzibar Dk.Shein. azungumza na Viongozi wa Wizara ya Elimu Ikulu.
STATE HOUSE ZANZIBAROFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 17.5.2012
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeeleza kuwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Tunguu umekamilika kwa asilimia 90 ambapo Mkandarasi ameahidi kukamilisha kazi yote na kukabidhi majengo katika mwezi wa Julai mwaka huu.
Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali ulieleza hayo leo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.
Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo ambapo Mwenyekiti wake ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ambapo pia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alihudhuri pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Abdulhamid Yahya Mzee.
Katika maelezo yake uongozi huo ulieleza kuwa kazi zinazoendelea hivi sasa ni pamoja na upakaji rangi na uchongaji wa madirisha, milango na makabati pamoja na kutengeneza bustani.
Aidha, Uongozi huo chini ya Waziri wake Mhe. Ali Juma Shamuhuna, umeeleza kuwa katika kukabiliana na tatizo la udanganyifu kwa wanafunzi watahiniwa, Wizara hiyo inakusudia kuimarisha usimamzi wa maskuli kwa kuimarisha ukaguzi wa skuli, mafunzo ya uongozi kwa waalimu wakuu na mafunzo kazini kwa walimu.
Pia, Wizara inakusudia kuanzisha mitihani ya pamoja ya majaribio kwa wanafunzi wa Darasa la Saba, Kidato cha Pili, Kidato cha Nne na Kidato cha Tano ambapo wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na mchepuo watafanya mitihani ya Kidato cha Pili na watakaoshindwa watarudia masomo ya Kidato cha Pili sawa na wale wa kidato cha Tano.
Ili kuongeza idadi ya walimu wa sayansi na hisabati kwa skuli za sekondari, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kimeanzisha darasa la Kidato cha Tano kwa masomo ya sayansi ili wanafunzi wanaomaliza kidato cha Sita wajiunge na ualimu kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza.
Kwa maelezo ya Waziri Shamuhuna, Chuo hivi sasa kina jumla ya wanafunzi 35 katika kidato hicho ambapo pia, Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia ina mpango wa kuanzisha kozi maalum kwa ajili ya kuwashajiisha vijana kupenda masomo ya sayansi.
Wizara inakusudia kuendelea kujenga vyumba vya maabara na kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara kwa skuli za sekondari na msingi, hiyo ni kutokana na skuli nyingi hushindwa kufanya mazoezi ya vitendo kutokana na kutokuwa na maabara na vifaa vya kutosha.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa unakusudia kuimarisha vyuo vya Kiislamu nchini, Mradi ambao utaendelea na ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Kiislamu, Kiuyu, Pemba.
Pia, ujenzi wa uzio na ujenzi wa Msikiti Mkubwa wa Kisasa, madarasa, kumbi ya mikutano, kituo cha Kompyuta na kuzungusha uzio katika Chuo cha Kiislamu, Mazizini kwa kushirikiana na Serikali ya Oman.
Wizara hiyo ilieleza kuwa, kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, inakusudia kuendeleza na utekelezaji wa MKUZA II na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu (ZEDP) na Sera ya Elimu ya mwaka 2006 ambapo Wizara itahakikisha kuwa malengo ya Milenia na Elimu kwa wote yanafikiwa ifikapo mwaka 2015.
Dk. Shein kwa upande wake alieza haja ya kuendeleza kuwasomesha vijana masomo ya sayansi na kuunga mkono mpango wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kwa kuanzisha utaratibu wa kuwasomesha vijana kwa lengo la kuongeza waalimu wa sayansi.
Alielesema kuwa imefika wakati kwa Wizara ya Elimu kuongeza juhudi na kuchukua hatua za makusudi katika kuwatayarisha na kuwaelekeza katika masomo ya sayansi tokea wakiwa skuli ili baadae waweze kuwa wataalamu katika fani mbali mbali za sayansi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliutaka uongozi huo wa Wizara ya Elimu kuwahamasisha zaidi kusoma masomo ya sayansi hasa watoto wa kike sanjari na kuwa karibu na wazee wao ili waweze kuwapa msukumo watoto wao ili wayapende zaidi masomo ya sayansi.
Dk. Shein pia alitoa maagizo kwa Wizara hiyo kulifanyia kazi suala la kuweka mazingira bora kwa daghalia za hapa nchini ili ziweze kutoa huduma zake vizuri kwa wanafunzi kama ilivyokuwa siku za nyuma na kuweza kusoma kwa ufanisi zaidi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha (SUZA) kuanza taratibu za kuhama mara watakapokabidhiwa majengo hayo mapya ili mwaka wa masomo utakapoaza wanafunzi waweze kuanza masomo yao bila ya usumbufu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Pamoja na mikakati mizuri ya serikali ktk kulitafutia ufumbuzi suala la elimu visiwani, ipo haja kwa serikali kufanya mambo yafuatayo;
ReplyDelete1.Skuli ya lumumba itengwe maalum kwa masomo ya sayansi tu na sio vinginevyo.
2.SUZA, ianzishe kitivo maalum cha kiswahili na kuimarisha kile cha komputa ambacho kinaanza kuonesha mafanikio tokea kuwasili kwa prof. Rai
3. Wakati umefika kwa serikali kubadili kilichokua chuo cha ualimu Nkrumah ili nacho kiweze kuwa chuo kikuu cha utalii ambacho kitaweza kuandaa wataalamu wa sekta hiyo pamoja na kuvutia wanafunzi wa kigeni.
4. Serikali ifikirie pia fani nyingine muhimu sio kung'ang'ani ualimu tuu kamailivyo kua miaka ya nyuma.