STATE HOUSE ZANZIBAR OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.5.2012
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa licha ya mfumko wa bei za vyakula kuwa juu lakini bado Zanzibar kuna unafuu ikilinganishwa na nchi nyengine jirani za Afrika Mashariki.
Dk. Shein alisema kuwa hiyo inatokana na Sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupunguza kodi za vyakula pamoja na kuwepo kwa makubaliano baina ya Wizara ya Biashara na Wafanyabiashara katika kupanga bei za vyakula hali ambayo inaenda vizuri.
Hayo aliyasema leo wakati Dk. Shein alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.
Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Abdulhamid Yahya Mzee.
Katika maelezo yake na uongozi huo Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na Sera hiyo ya Serikali pamoja na makubaliano hayo hali ambayo imeleta unafuu wa bei huku akisisitiza haja ya kutilia mkazo katika kuanzishwa viwanda vya kutengeneza bidhaa ambazo zitauzwa nje ya nchi.
Alisema kuwa mikakati maalum imewekwa katika mipango kazi pamoja na kuimarisha maeneo ya kiuchumi
Akieleza juu ya zao la karafuu, Dk. Shein alisema kuwa changamoto iliyopo kwa siku za usoni katika kuliimarisha zao hilo inapaswa zikaanzwa hivi sasa huku akieleza kuwa serikali itaendelea na msimamo wake ule ule wa bei iliyoiweka ya ununuzi wa karafuu kwa wananchi.
Nao uongozi wa Wizara hiyo chini ya Waziri wake Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, ulieleza kuwa katika suala la kusimamia bidhaa za mchele na sukari zisivuushwe nje ya Zanzibar kwa magendo, Wizara hiyo kwa kushirikiana na KMKM imeimarisha ulinzi maalum katika bandari za Zanzibar
Wizara hiyo ilieleza kuwa kwa kushirikiana na KMKM imefanikiwa kukamata jumla ya paketi 1,375 za mchele na paketi 111 za sukari, ambazo zilikuwa zinasafirisha kwenda nje ya Zanzibar kwa kutumia jahazi. Uongozi huo ulieleza kuwa hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa usafirishaji wa bidhaa hizo kwa magendo na kukwepa kulipa kodi na kuikosesha serikali mapato yake.
Aidha, Wizara hiyo imeendelea na hatua za kusimamia mwenendo wa bei za bidhaa muhimu za chakula na kuhakikisha kwamba bei hazivuki kiwango cha bei kilichokubaliwa.
Katika kipindi cha mwezi Januari-Machi 2012 bei za mchele wa kawaida na sukari zilipungua kidogo katika soko la dunia na katika soko la Zanzibar na kueleza kuwa, hivi karibuni kumeanza kupanda tena kwa bei za bidhaa muhimu hasa mchele.
Uongozi huo ulielez kuwa katika kipindi cha Mwezi Machi-Aprili 2012 kumejitokeza wimbi la kusafirisha bidhaa za mchele wa kawaida na sukari kwenda nje ya Zanzibar kimagendo kutokana na bidhaa hizo bei yake kuwa juu ikilinganishwa na bei katika soko la Zanzibar.
“Kwa mfano bei ya jumla ya mchele wa kawaida katika soko la unauzwa kati ya Tsh. Tsh 50,000-52,000 kwa kilo 50 wakati Dar-es-Salaam unauzwa kati ya Tsh 72,000-75,000”,alisema Waziri Mazrui
Kwa upande mwengine uongozi huo wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kwa biashara ya karafuu, ulieleza kuwa tokea kuanza kwa msimu wa karafuu 2011-212 hadi kufikia tarehe 8 Mei 2012 Serikali imeshanunua jumla ya tani 4,782.877 za karafuu zenye thamani ya T.Shs 71,555,3222,250.
Wizara hiyo ilieleza kuwa maandalizi ya kuanza mchakato wa kuipatia utambulisho maalum (Branding) karafuu ya Zanzibar unaendelea vizuri.
Uongozi huo ulieleza kuwa pamoja na hatua za kujiimarisha katika masoko ya nje, hivi karibuni soko la karafuu ya Zanzibar limepiga hatua muhimu baada ya kupatiwa nafasi katika orodha ya mazao yatakayoondolewa kodi chini ya Mapango wa Serikali ya India wa ‘Duty Free and Tariff Preference Scheme-DFTP’.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Waziri wake Mhe. Abubakar Khamis ambapo uongozi huo ulieleza jinsi ulivyojikita katika maeneo ya MKUZA, Dira 2020, utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu na suala zima la bajeti yake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment