Habari za Punde

Dk Shein Akutana na Watendaji Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya VijanaDk n

STATE HOUSE ZANZIBAR OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.5.2012

WIZARA ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto kwa niaba ya Wanawake wote pamoja na kina Baba, wametoa shukurani za dhati kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Moahmed Shein kwa tamko lake la kufuta ada za uzazi kwa akina mama wote watakaokwenda kujifungua katika hospitali za serikali.

Uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto ulieleza hayo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.

Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar uliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pia, ulihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Uongozi huo, ulieleza kuwa hilo ni jambo kubwa sana ambalo litawasaidia wakina mama, litanusuru vifo vya mama na watoto kwa kiwango kikubwa sana kutokana na hatua ya Rais Dk. Shein kutoa tamko hilo na kuamua kwamba gharama hizo zitabwebwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Aidha, uongozi huo ulitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa uwamuzi wake wa kufanya ziara rasmi ya kutembelea nyumba za Wazee Sebleni na kuzungumza na wazee.

Walieleza kuwa kitendo chake hicho kinaonesha mapenzi makubwa na imani aliyonayo Dk. Shein kwa wazee”Kwetu sisi jambo hili ni faraja kubwa sana kwani tumefarajika na wazee wetu wamefurahi sana” ilisema taarifa iliyosomwa na Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Bi Zainab Omar.

Bi Zainab alieleza kuwa kutokana na ujio huo wa Rais Dk. Shein wameweza kupata mafanikio makubwa na kuweza kutatua matatizo makubwa ambayo wao yangewakwaza yakiwemo tatizo la maji katika nyumba hizo za wazee, ulinzi kwa wazee, usafiri wa gari kwa wazee na huduma ya chakula lwa wazee sanjari na huduma za afya.

“Yote haya yamewezekana kutokana na moyo wako safi wa kuwatumikia na kuwasaidia wazee, sote sisi tunakushukuru sana”alieleza Bi Zainab.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa umeanza hatua za ukarabati wa umkumbi na ujenzi wa jiko la kisasa kwa ajili ya kutoa huduma za chakula kwa Wazee wa Sebleni ambapo pia, utaratibu kama huo unafanyika huko Limbani Pemba kwa ajili ya Wazee walioko Pemba.

Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa umeendelea kuwapatia hifadhi na huduma bora watoto wanaolelewa katika nyumba za Serikali ikiwa ni pamoja na kutiliana saini Mkataba wa Mashirikiano na Shirika lisilo la Kiserikali la kulea watoto SOS katika Mradi mkubwa wa Shirika hilo ambao utatekelezwa kisiwani Pemba na utawasaidia watoto na familia zao zenye mazingira magumu.

Kwa maelezo ya Waziri huyo, Wizara imetoa misaada mbali mbali kama vile vyarahani na fedha taslim kwa ajili ya kuwasaidia wakina mama ambao wameonyesha juhudi kubwa katika masuala ya kujiondoshea umasikini kwa kufanya kazi za kilimo, ushoni, ufugaji, ufinyanzi, ususi na kazi za mikono wanazofanya ili kupambana na haliya maisha.

Uongoni huo ukieleza juu ya suala la unyanyasaji na udhalilishaji wa Watoto kijinsia ulisema kuwa bado unaendelea kwa upande wa Unguja na Pemba na kueleza kuwa wazee wa watoto katika jamii bado hawajatoa ushirikiano wa kutosha pamoja na elimu inayotolewa kila mara juu ya suala hilo.

Uongozi huo pia, ulieleza kuwa umeendelea kuwasaidia vijana kwa kuanzisha shamba la upandaji wa maua na mbogamboga shughuli ambazo zinatekelezwa Unguja na Pemba.

Wizara hiyo ilieleza kuwa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Vijana wa (ZASOSE) imekuwa ikifanya juhudi za pamoja za kuwatafutia ajira za muda na za kudumu vijana ambao tayari wamejikusanya pamoja katika makundi ya fani ya kazi tofauti.

Nae Dk. Shein kwa upande wake aliipongeza Wizara hiyo kwa mafanikio iliyoyapata na kuitaka kuyaeleza kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ili wapate kuelewa juhudi za serikali yao kupitia Wizara hiyo.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za haraka agizo lake juu ya mlo wa wazee wa kutwa mara tatu kama alivyolitoa katika ziara yake wakati alipowatembelea wazee wanaoishi katika nyumba za Wazee, Sebleni.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa kuna haja ya kuwepo mashirikiano ya pamoja kati ya Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika pamoja na Wizara hiyo katika kuendeleza mchakato wa kuanzisha Soko la Jumaapili la Wajasiriamali huko kiwiwani Pemba.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.