Na Joseph Mwambije, SONGEA
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Nape Nnauye amesema serikali itawachukulia hatua za kisheria ikiwemo na kufukuzwa kazi watendaji wabovu kwani kuendelea kuwepo serikalini wanakichafua chama.
Nape alisema wananchi waliingia mkataba na CCM kwa kukichagua kwenye uchaguzi mkuu uliopita, hivyo kuendelea viongozi wabovu watambe ni kuharibu mkataba baina ya wananchi na CCM.
Alisema kutokana na hali hiyo, CCM hitakubali kuona inawatendaji wabovu kwani athari zao zitahatarisha wananchi washindwe kuingia mkataba na CCM wakati wa uchaguzi utakapowadia.
Nape alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wanaCCM na wananchi kwenye hafla iliyofanyika katika kiwanja cha Zimamoto kilichopo Manispaa ya Songea.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, alisema kuendelea kuwa na watendaji wabovu serikalini ni kukichimbia kaburi chama hicho, jambo ambalo kwa sasa halitavumiliwa.
Nape alisema mawakala waliochakachua vocha za pembejeo za kilimo kwa kushirikiana na watumishi wa serikali kwa pamoja watafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na kwamba watendaji wa kata, mitaa na vijiji walioiibia serikali nao hawatakwepa mkondo wa sheria.
Aliitaka halmashauri ya Manispaa ya Songea katika kitengo chake cha Idara ya Ardhi na Mipango miji, kucha tabia ya kuchakachua viwanja kwa kuuza kiwanja kimoja zaidi ya mtu mmoja pamoja na kupora viwanja.
Aliwaonya wakurugenzi wa halmashauri na kuwataka kuacha kuiibia serikali kwani hivi sasa iko macho na wakurugenzi wa aina hiyo wanaweza kufungwa jela ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kuiibia serikali.
Akizungumzia operesheni ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya vua gamba vaa gwanda, alisema kuwa wanachopaswa kufanya ni kuhubiri uzalendo kwa kuwa suala la uzalendo si la itikadi bali ni la uzalendo na kwamba mtu anaweza akavua gamba na kuvaa gwanda na akaendelea kuwa mwizi.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, alisema chama chake kitaendela kubaki madarakani kutokana na kujiwekea mfumo wa kupunguza matumizi ya serikali kwa kumuongezea nguvu mkaguzi mkuu wa serikali (CAG) kwa kumpatia vifaa na ofisi.
Alibainisha kuwa vyama vya upinzani havina uchungu na nchi ndio maana viongozi wake wamekuwa wakisikika mara kwa mara wakisema wasipoingia madarakani damu itamwagika.
"Vyama vya upinzani ni makundi ya wanaharakati na chama cha siasa ni kimoja nacho ni CCM, kwa sababu hiyo wamekuwa hawana uchungu na nchi wanatoa kauli za kuvunja amani hebu waende wakaone katika nchi za Sudani, Eritrea, Libya, Somalia, Ethiopia na nchi nyengine ambazo hazina amani jinsi watu wake wanavyoteseka", alisema Nape.
No comments:
Post a Comment