Habari za Punde

Waziri Aagiza Muwekezaji Kunyang’anywa Hoteli


Na Bakari Mussa, PEMBA


WAZIRI wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, amelitaka Shirika la Hoteli za Serikali, kuinyang’anya kampuni ya National Marketing hoteli ya Wete.

Waziri huyo ametaka ichukuliwe haua hiyo kufuatia kampuni hiyo iliyokodi hoteli hiyo ya serikali kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba wa ukodishwaji.

Waziri Mbarouk ametoa agizo hilo huko Wete kisiwani Pemba, wakati alipoitembelea hoteli hiyo akiwa kwenye ziara ya kuzitembelea Idara ya Taasisi zilizondani ya wizara hiyo kisiwani humo.

Alisema kampuni ya National Marketing, iliyokodishwa hoteli hiyo imeshindwa kuiendeleza na kuwa katika hali mbaya ikiota miti pamoja na kuvujiwa.

Waziri huyo alibainisha kuwa asingependa kuona fedha za umma zilizotumika kujengelea hoteli zinapotea kwa uzembe wenye kisingizio cha uwekezaji.

"Hii ndio kauli yangu, nasema arejeshe hoteli hii, siwezi kuona fedha za Wananchi zikipotea namna hii", alieleza.

Nae Mkurugenzi wa Shirika hilo, Sabah Saleh Ali, alisema shirika hilo lilitangaza zabuni ya ukodishwaji wa hoteli hizo za serikali kwa vile walikuwa hawawezi kuzihudumia na hivyo mwaka 2004, wakaikodisha kampuni hiyo kwa masharti ya kuiendeleza ambapo wameshindwa kufanya hivyo.

Aidha mmoja wa wasimamizi wa hoteli hiyo kutoka kampuni ya National Marketing, Lela Nassor, alifahamisha kuwa ni kweli walikodi hoteli hiyo tokea mwaka 2004, lakini wameshindwa kufanya lolote.

Katika Ziara hiyo ya kutembelea taasisi zilizomo ndani ya Wizara ya Habari, Waziri huyo aliitaka Radio Jamii iliyoko Micheweni, kuitumia Radio hiyo kutoa taaluma mbali mbali ambazo zitaisaidia jamii hiyo ya Micheweni kuondokana na umasikini.

Alisema kuwa jamii ya watu wa Micheweni itakapo changamkia taaluma mbali mbali zinazotolewa na kituo hicho ikiwemo ufagaji, uvuvi na kilimo ni wazi kuwa uaskini utapungua kwa kiasi kikubwa.

Alisema ni wakati kwa wataalamu kuwafundisha wananchi wa Micheweni ili waweze kuwa na taaluma kwa wananchi ili mipango ya kutokomeza umasikini iweze kufikiwa.
Alizitaka taasisi zinazotumia kituo hicho cha Radio Jamii kukitumia kituo hicho kwa kutoa matangaazo yao na sambamba na kuyalipia ili kituo kiweze kujiendesha.

Akizungumzia Utalii katika maeneo ya Micheweni, alisema kuwa hadi haulijapewa kipao mbele na kuitaka mikakati iwekwe ili sekta hiyo iwe mojawapo katika kuinua maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Waziri huyo alisema Micheweni imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, lakini bado havijatumika na kusisitiza kuwa vivutio hivyo vibainishwe ili eneo hilo liwe moja ya vituo muhimu vya kiutalii nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.