Na Othman Khamis Ame, OMKR
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema Taifa la Tanzania linaweza kuwa katika misuko suko isiyokwisha endapo suala la matatizo ya Kifamilia linaloonekana kuikumba Jamii litaachiliwa kuendelea.
Akifungua Kongamano la Wanawake waombolezao kwa ajili ya Taifa liliofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kikristo kilichopo Zinza Jijini Dar es salaam Mama Asha alisema matatizo ya kifamilia hivi sasa yameongezeka na kutishia Taifa.
Mama Asha alisema Familia imara hujenga Taifa Imara lakini hilo litapatikana kama nguvu za upendo zitapewa nafasi kubwa zaidi katika familia hizo.
“ Hakuna jawabu ya mkato ya kujenga familia imara lakini uzoefu unaonyesha kuwa ‘upendo’ husaidia kwa asilimia kubwa kujenga familia imara ambayo hatimae huweza kukabiliana na matatizo yanayojitokeza kwa ufanisi zaidi”. Alifafanua Mama Asha.
Mama Asha alifarajika kuona miongoni mwa mambo yaliyozunguzwa katika kongamano hilo ni matatizo ya Familia.
Alisema mategemeo yake ni kuona Kongamano hilo litasaidia kutoa mafunzo bora ya kujenga Familia zenye upendo ambazo kwa mtizamo uliopo ndizo zenye nafasi ya kukabiliana na matatizo yaliyopo na yajayo ndani ya Jamii.
Ameupongeza Uongozi wa New Millenium Group kwa kuandaa Kongamano hilo lililowaunganisha Washiriki kutoka sehemu mbali mbali ndani na Nje ya Nchi bila ya kujali Dini na Itikadi zao.
Alisema hilo ni Kongamano linalofananishwa na ule Mshikamano unaofafanuliwa kila mara na Viongopzi wa Kisiasa na Kidini unaolenga kupiga vita Umaskini, Ujinga na Maradhi.
Aliwataka wana Jumuiya hiyo ya New Millenium Group kuendelea kuliombea Taifa hili la Tanzania kunusurika na majanga, Maradhi na Maafa ambayo yameshuhudiwa kuathiri baadhi ya Mataifa hapa Duniani.
Katika Risala yao wana Jumuiya hiyo ya New Millenium Group Tanzania wamewaomba Wananchi wote wasitosheke na Ibada badala yake wajitahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili Taifa liondokane na Umaskini, Ujinga na Maradhi.
Walisema akina Mama wakitumia vyema nafasi walizokuwa nazo wana mchango mkubwa wa kuleta mabadiliko ndani ya Jamii inayowazunguuka.
Hata hivyo walikumbusha kwamba Taifa bado linakabiliana na matatizo ya Umaskini, Maradhi, rushwa na ukosefu wa Maadili kwa baadhi ya Viongozi ambayo kuyapiga vita ni jukumu la watu wote.
Kongamano hilo la siku tatu limehudhuriwa na takriban washiriki 570
Hapa Nchini na kushuhudiwa pia na wawakilishi kutoka Mataifa ya Afrika Kusini, Zimbabwe, Zambia, Marekani na Botswana.
Wengine ni Nchi Jirani kutoka Kenya Uganda, Malawi na wenyeji Tanzania.
Taifa mashakani kama vijana wanaomaliza vyuo hawataajiriwa Zanzibar!
ReplyDelete