Habari za Punde

Choo Uwanja wa Ndege Hakijamalizika tokea 2005!


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliagiza kukamilishwa mara moja kwa Choo Maalum kwa ajili ya udhibiti wa uingizwaji wa Dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Kitengo cha kuzuia Dawa haramu za kulevya Mrakibu Msaidizi Muandamizi wa Polisi Kamanda Mkadam Khamis Mkadam. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Fatma Abdullhabib Fereji. 

Picha na Saleh Masoud Mahmoud

Na Othman Khamis Ame

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikagua choo Maalum kwa ajili ya Watu wanaoshukiwa kuingiza Dawa za kulevya hapo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar. 

 Mkuu wa Kitengo cha kuzuia Dawa haramu za kulevya Mrakibu msaidizi muandamizi wa Polisi Kamanda Adam alimueleza Balozi Seif kwamba mataumizi ya choo hicho yataanza mara baada ya kukamilika kwa uwekaji wa vipoza hewa ambavyo ni muhimu kwa mazingira ya sehemu hiyo. 


 Kamanda Mkadam Khamis Mkadam alisema ujenzi wa choo hicho ulioanza tokea Mwaka 2005 umegharamiwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa { UNDP } kupitia Ofisi ya muendesha Mashataka Zanzibar. 

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliuagiza Uongozi unaosimamia Ujenzi huo kuhakikisha kwamba Ujenzi huo unakamilika mara moja. 

Balozi Seif alisema utaratibu ni vyema ukafuatwa wa kazi hiyo na kupendekeza apelekewe makisio ya gharama zilizobakia ndani ya Wiki moja ili matarajio ya matumizi ya choo hicho kwa lengo la udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini lifikiwe. “ imekuwa hadithi Choo hichi tokea Mwaka 2005 kwa karibu miaka saba sasa kwa mwenendo huu hata wale waliotusaidia gharama za kazi hii watatuona Watu wa ajabu kweli kweli kwamba choo hakishi”. Alifafanua Balozi Seif Ali Iddi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.