Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiwa katika Ziffa { Maandamano} ya Amani ya kusherehekea miaka 50 tokea kuanzishwa kwa Al Madrasat Shamsiyah Mkoani Tanga ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiuhutubia Umati mkubwa wa Waumini wa Dini ya Kiislamu kutoa Mikoa mbali mbali Nchini waliohudhuria Maadhimisho ya Kutimia Miaka 50 tangu kuasisiwa kwa Al Madrasat Shamsiyah ya Mkoani Tanga Mwaka 1962.
Picha na Saleh Masoud Mahmoud
Na Othman Khamis Ame
Wazazi na baadhi ya Masheikh Nchini wameaswa kuachana na tabia ya kuwafundisha Vijana hulka ya kuvunja Amani Miongoni mwa Jamii kwa kisingizio cha shetani.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiuhutubia umati mkubwa wa Waumini wa Dini ya Kiislamu uliohudhuria Maadhimisho ya Miaka 55 tokea kuanzishwa kwa Taasisi ya Walimu wa Kiislamu Tanzania { TAMTA } NA Miaka 50 ya Almadrasat Shamsiyah Mkoani Tanga.
Balozi Seif alisema Tanzania yenye Amani ndiyo itakayowawezesha wana Jamii na Waumini kuabudu kwa Utulivu kama ilivyoamrishwa kwenye Vitabu vya Dini.
Alifahamisha kwamba Waumini wa Dini ya Kiislamu wanapaswa pia kuzingatia Utiifu ili kuendeleza Taasisi zao vyenginevyo zitaendelea kubakia nyuma kila wakati. Balozi Seif aliipongea Taasisi hiyo ya Tamta kwa ujasiri wake wa kuwa chem. Chem ya Elimu ya Dini na kuiomba iendelee kuelimisha Waumini na Jamii katika kufuata nguzo ya Kiislamu.
“ Mbegu mliyoipanda miaka 50 iliyopita ikachipua, kukua na kutoa Matunda ambapo kila msimu unapowadia mnavuna Matunda ambayo huliwa sehemu mbali mbali za ardhi ya Tanzania na baadhi ya Nchi Jirani”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliikumbusha Jamii kuhakikisha kwamba changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Tamta zinapatiwa ufumbuzi kwa kutumia njia ya Ushirikiano na Umoja.
Alisema ulipati wa ada usiowakuridhisha wa Wazee ambao watoto wao wanapatiwa Elimu katika Taasisi hiyo ni aibu ikizingatiwa na mafundisho ya Dini ambayo ni sawa na kuitenga Jumuiya ya Kiislamu.
Katika Kuunga mkono Juhudi za kutatua changamoto zinazoikabili Madrasa hiyo ya Shamsiyah Balozi Seif Ali Iddi ametoa zawadi ya Shilingi Miilioni 1,000,000/- Taslimu kusaidia harakati za ujenzi wa Mabweni ya Madarasa hiyo.
Akisoma Risala ya Taasisi hiyo Katibu Mkuu wa Tamta Sheikh Mohd Abdull Zikri alisema Madrasa ya Shamsiyah haiendeshwi kifaida hali ambayo imepelekea uendelezaji wake hukumbwa na Changamoto.
Sheikh Mohd Abdull amewaomba Wafadhili kuendelea kuongeza nguvu za uchangiaji kwa lengo la kuijengea uwezo wa kiuendeshaji Madrasa hiyo ya Kiislamu.
Mapema akikariri moja yha hadhithi mashuhuri inayoelezea upendo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi alisema yamethibiti Mahaba kwa waja wanaotembeleana kwa ajili ya Mwenyezi Muungu.
Sheikh Kabi aliuomba Uongozi wa Madrasat Shamsiyah kuendelea kudumisha Tabia hiyo njema ya kuwa karibu na Waumini wa Sehemu mbali mbali jambo ambalo huongeza nguvu ya upendo miongoni mwa Waumini wa Dini ya Kiislamu.
Sherehe hizo zilizoambatana na kunadiwa kwa Keki iliyotengenezwa na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania { JUWAKITA } kwa lengo la kutunisha mfuko wa Madrasa hiyo ambayo ilifikia gharama ya Shilingi Milioni 2,000,000/- zilizotolewa na Sheikh Sharif Muhana Mwinyibaba kutoka lamu Mombasa Nchini Kenya.
Mnada huo ulichangiwa pia na baadhi ya Waumini wa Dinin hiyo walioshiriki Maadhimisho hayo. Balozi Seif pamoja na mambo mengine pia alipokea Maandamano ya amani ya kusherehekea Elimu ya Dini { Zaffa } na kushirikisha Madrasa Kadhaa kutoka mikoa Mikoa mbali mbali ya Tanzania chini ya Matawi ya Jumuiya ya Tamta.
No comments:
Post a Comment