Umati mkubwa wa Wakaazi wa Kata ya Kimara Wilaya ya Kinondoni Mkoa Dar es salaam waliohudhuria sheehe za kukabidhiwa vifaa kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kata hiyo vilivyotolewa msaada na Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi wa Kata hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi baadhi ya Vifaa vya Hospitali Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Kimara Dr. Alphoncina Mbinda. Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi 5,189,000/- vimetolewa msaada na Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Kimara Wilaya ya Kinondoni Mkoa Dar es salaam.
Na Othman Khamis Ame OMKR
Mabadiliko ya Maadili mema katika Jamii na Taifa yataendelea kuwepo endapo Jumuiya ya Wazazi itajihusisha zaidi na mapambano dhidi ya vitendo viovu vinavyofanywa na kundi kubwa la Vijana hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo katika hafla fupi ya kukabidhi Vifaa vya Hospitali kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kata ya Kimara vilivyotolewa na Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi wa Kata hiyo iliyopo Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam.
Balozi Seif alisema Jumuiya ya Wazazi ilipewa jukumu na Taifa la kuendeleza Malezi na Elimu bora ingawa zama hizi jukumu hili ni mzigo mzito kutokana na kuporomoka kwa Maadili katika Jamii.
Alisema Jamii hivi sasa imegubikwa na vitendo vya Ujambazi, Wizi, Ubakaji na hata utumiaji wa dawa za kulevya mambo ambayo yanaviza juhudi za ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisisitiza Wazazi hao kuchukuwa juhudi za ziada katika kuzuia machafu hayo ili Jamii iwe na Taifa imara na lenye Kuheshimika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wazazi kwamba Taifa bado lina changa moto kubwa kutokana na kuenea kwa maambukizu mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Hivyo aliwasisitiza kusimamia mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi hivyo ambavyo ni vyema yakawa ya kudumu sambamba na upimaji wa hiari ili watu waelewe afya zao.
Akizungumzia suala la Mazingira Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Jumuiya hiyo ya Wazazi kwa kuihimiza Jamii kutunza na kuhifadhi mazingira katika ngazi ya Familia. “ Hili ni jukumu lenu kwa vile nyinyi ndio wahamasishaji wazuri wa wazazi katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira”. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Katika kuunga mkono juhudi za Jumuiya hiyo ya Wazazi kata ya Kimara Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameahidi kutoa mchango wa shilingi 1,000,000/- zitakazosaidia uendelezaji wa ununuzi wa Vifaa vya Kituo hicho cha Afya cha Kimara.
Akitoa Taarifa fupi ya Kituo cha Afya cha Kimara Wilaya ya Kinondoni Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Dr. Alphoncina Mbinda alisema Hospitali hiyo inahudumia zaidi ya Wagonjwa 500 kwa siku katika Tiba za chanjo, huduma za mama na watoto, Maabara pamoja na huduma za ushauri nasaha kiwango ambacho ni kikubwa kuliko uwezo wa kituo chenyewe.
Dr. Alphoncina alizielezea baadhi ya changa moto zinazokikabili kituo hicho ikiwa ni pamoja na Jengo dogo la Hospitali,Watumishi wachache pamoja na ukosefu wa gari ya huduma. Hata hivyo Dr. Alphoncina aliushukuru Uongozi wa Wazazi Kata ya Kimara kwa uamuzi wake wa kutoa Msaada wa Vifaa hivyo ambao kwa kiasi Fulani utasaidia kupunguza matatizo kwa hatua kubwa.
Akimkaribisha Balozi Seif Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Mh. Amina Mabrouk aliwaasa Vijana hasa Wanawake kujiepusha na tabia ya kuacha maeneo ya mwili wao wazi. Mh. Amina alisema tabia hiyo kwa kiasi kikubwa huchangia wimbi la udhalilishwaji kijinsia ambapo wengi kati yao kujikuta wakiambukizwa maradhi ya uasherati.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi 5,189,000/- ni pamoja na Kitanda cha Wagonjwa, Mizani, Screen, Mashine ya kupimia Umonjwa wa Moyo pamoja na Viti vya kuchukulia Wagonjwa.
No comments:
Post a Comment