Habari za Punde

Moyo, Shamsi wavutana suala la Muungano


Na Mwinyi Sadallah

Mwanasiasa Mkongwe Zanzibar Hassan Nassor Moyo, amesema kwamba wakati mazungumzo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanafanyika, Msaidizi Mkuu wa Rais wa Kwanza Zanzibar, Salum Rashid alikuwa kwa kinyonzi akinyoa ndevu zake.

Tamko hilo amelitoa wakati akiwasilisha mada kuhusu uzoefu wa viongozi waliopita katika masuala ya Muungano katika semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) huko Chukwani Zanzibar jana.


Alisema kwamba Rashid, alikuwa Katibu Mkuu (Ikulu) wakati wa uongozi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Sheikh Abeid Amani Karume, baada ya kumuondoa katibu wake kutokana na kuhudhuria mazungumzo hayo akiwa hajanyoa ndevu zake.

Alisema Aprili 14, 1964 aliyekuwa Rais wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alimwita Rais wa Zanzibar Ikulu ya Dar es Salaam, kufungua mazungumzo ya mpango wa Muungano wa Tanganyika Zanzibar.

Hata hivyo alisema baada ya Karume kufika Ikulu alimkuta msaidizi wake amewasili akiwa hajashevu ndevu na kumtaka achukue gari na kwenda kwa kinyonzi.

“Baada ya kurudi kutoka kushevu ndevu kwa kinyonzi alikuta wanaendelea ndani na mazungumzo lakini kwa kuzingatia itifaki hakuweza kuingia ndani.”alisema Mzee Moyo.

Alisema kwamba Aprili 22, mwaka huo Mwalimu Nyerere alikuja Zanzibar kukamilisha mazungumzo ya Muungano lakini wasaidizi wake wa muhimu mzee Karume aliwatenga na kuwaweka katika ‘korido’ wakati waziri wake wa Nchi Ofisi ya Rais wakati huo Aboud Jumbe Mwinyi akiwa safari ya kikazi Pemba.

“Baada ya mazungumzo Karume alimwita msaidizi wake Salum Rashid na kumpatia waraka wa muungano amsomee kifungu kwa kifungu na kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu ulikuwa umeandikwa kizungu kabla ya kusainiwa”. 

Hata hivyo alisema Mjumbe wa BLM Khamis Abdallah Ameir, alitaka kufahamu kwa nini mpango huo unafanyika harakaharaka lakini Karume alimuondoa wasiwasi na kuwaeleza wajumbe kama hawataki yupo tayari kumrejeshea makaratasi yake Nyerere lakini Wajumbe wote waliunga mkono mpango wa Zanzibar kuungana na Tanganyika.

Alisema Baraza la Wawakilishi (BLW) lina mamlaka kamili ya kukubali kuendelea kuwepo kwa Muungano au kukataa kwa sababu ni chombo cha wananchi kama Baraza la Mapinduzi Zanzibar (BLM).

Moyo alisema kwamba chimbuko kubwa la muungano huo ulitokana na hofu ya vitisho vya Zanzibar kupinduliwa iliyokuwa ikitolewa na baadhi ya viongozi kutoka Afrika Mashariki.

Moyo alisema kero za Muungano zimeanza kuibuka muda mrefu na kutoa mfano mwaka 1970 kulitokea kishindo baada ya Zanzibar kupendekeza waraka wa kutaka baadhi ya mambo kurekebishwa katika orodha ya mambo ya Muungano ikiwemo kuondoa Jeshi la Polisi.

Wajumbe waliochangia mada hiyo ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye alivutana kwa muda mrefu kutaka maelezo ya kina, Hamza Hassan Juma, (Kwamtipura) Ismail Jussa ladhu, (Mji Mkongwe) Makame Mbarouk Mshimba (Kitope) Salim Abdalla Hamad, (Mtambwe) na Fatma Mbarouk, (Amani).

Hata hivyo Mzee Moyo, alishindwa kujibu maswali mazito ya Nahodha aliyetaka kujua kwa nini nafasi ya Zanzibar kiulinzi na kiusalama iwe nje ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Shamsi alisema kwamba miaka 7 baada ya Mapinduzi Zanzibar kumefanyika majaribio 14 ya kutaka kuinagusha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Semina hiyo imeandaliwa na Baraza la Wawakilishi (BLW) na kudhaminiwa na serikali ya Norway, ambapo pia elimu juu ya Katiba inatarajiwa kutolewa katika majimbo 50 ya Zanzibar.

Chanzo: Nipashe Jumapili

3 comments:

  1. Mwinyi Sadalla sisi tunamfahamu sana, ni mtu ambaye daima asingependa Zanzibar kuwa na maendeleo yake dhidi ya Tanganyikam kutokana na asili yake!!

    ReplyDelete
  2. mzee moyo huuyu tumjuwae wachanganishwe bunge wote wa tanzania pamoja na kikwete pamoja na waandishi wahabari mwenye asili ya tanganyika hawana umwezombele na mwanamapinduzi nasor moyo nahoza siyo mwanasiasa nahodha ni mwalimu wa lukha ya kifaransa kwa chekecheya

    ReplyDelete
  3. Wakina Mzee Moyo hawana jambo jipya la kutueleza! Wameshatumia muda wao na sasa wanatakiwa wastaafu kwa amani wastuzingue!

    Mimi sidhani kama W'bari haja yao bado ni kujua namna muungano ilivyotokea, nadhani walio wengi tunataka kuona 'the way forward'

    La msingi ni vipi tunaweza kutatua kero zilizopo, ikiwa ni pamoja na hiyo fitna ya MAFUTA kama kweli yapo ili maisha yaendelee!!

    Kuhoji hoji mambo yaliyopita ni vizuri tu kama ni kwa ajili ya historia lkn vinginevo itatuletea shida!

    Leo utahoji Muungano ulivyotokea, kesho mapinduzi, kesho kutwa viongozi waliohusika, hatimae namna Waarabu walivyofika n.k.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.