(Innaa lillaahi Wainnaaa Ilayhi Raaji'uun: Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake YEYE tutarudi.... Quran Tukufu)
Jumuiya ya Mustakbal wa Zanzibar, MUWAZA, inaungana na Wazanzibari wenzao wa ndani na nje kutoa huzuni zake kubwa kwa msiba uliosababishwa na kuzama kwa meli ya Mv. Skaget siku ya Jumatano, tarehe 18.07.2012, karibu na Kisiwa cha Chumbe.
Wana MUWAZA wanaungana na Wazanzibari wenziwao wote kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote, wale ambao hadi sasa ndugu zao na jamaa zao hawajapatikana na wale waliojeruhiwa katika ajali hiyo ya kusikitisha.
Tunawaombea Rehema za Mwenyezi Mungu ziwafikie wote waliopoteza maisha yao katika janga hili, na wafiwa na waathirika wote tunawaombea Mwenyezi Mungu awape subra na imani katika wakati huu mgumu...Ameen.
Ilivyokuwa Zanzibar ni nchi ya visiwa na usafiri wa baharini wa Watu na bidhaa ni muhimu sana kwa maisha ya kila siku ya watu wake, serikali inawajibu wa kujenga hali na mazingira mazuri ili kuhakikisha ajali za kila mara za safari za baharini kutoka na kujia Zanzibar zinapungua sana.
Matukio kadhaa ya hivi karibuni ambayo roho za watu wengi na mali zilipotea au kuwa hatarini yamezidisha wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusu usalama wa safari za baharini. Ajali hizo zimechangiwa kwa sehemu kubwa na uzembe na kutokufuatwa barabara kwa kanuni tulizojiwekea.
Tunahisi kwamba dhamana kubwa na ya mwisho inaangukia mabegani mwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano wa Tanzania kujenga mazingira mazuri yenye kuhakikisha usalama wa hali ya juu wa safari za baharini kwa abiria na bidhaa. Dhamana hiyo haiwezi kuhamishiwa kwa wamiliki binafsi wa vyombo vya usafiri.
MUWAZA inasikitishwa sana kwa kukosekana uwiano mzuri baina ya Idara na Taasisi zinazohusika na kutoa taarifa za hali za hatari na za dharura pamoja na shughuli za uokozi wakati kunapotokea janga.
MUWAZA inasikitishwa sana na hali ya kukosekana vifaa vya kisasa vya kutumika wakati wa dharura. Suala hili ni muhimu na serikali inabidi ilipe kipaumbele cha mwanzo.
MUWAZA inatoa mwito kwa serikali ya Zanzibar ifanye uchunguzi huru na wa kina kujuwa sababu zilizopelekea kuzama kwa meli ya Mv. Skaget na wale watakaogunduliwa kuhusika na kusababisha janga hili wachukuliwe hatua za kisheria. Mkondo wa kisheria ufuate njia za uwazi na uadilifu wa hali ya juu, kila mtu akibakia hana hatia hadi itakapothibitika kinyume na hivyo.
MUWAZA inaziomba Serikali zote mbili, ya Zanzibar (SMZ) na ya Muungano zilifuatilie suala la kulipwa fidia watu walioathirika na janga hili kwa kuzingatia misingi ya haki na uwiano.
MUWAZA pia inachukuwa fursa hii kutowa masikitiko yake na kulaani vikali vitendo vya Jeshi la Polisi huko Zanzibar la kufyetua mabomu ya kutoa machozi na kurushia watu maji ya pilipili, hasa kuelekea kwa waumini waliokusanyika kwa njia ya amani ndani na nje ya Msikiti wa Mbuyuni /Zanzibar katika ibada ya kuwasomea dua ya maombolezi ndugu zao, Wazanzibari wenzao, waliopoteza maisha yao katika ajali ya Mv. Skaget. Vitendo vya utumiaji wa nguvu za mabavu ya Dola vilivyozusha ghasia na kizaazaa mitaani, Unguja mjini, havijakuwa na sababu ya lazima na vingeliweza kuepukika.
MUWAZA inapinga vikali vitendo vyovyote vya utumiaji nguvu na mabavu, visivyokuwa vya kisheria kutoka kwa vyombo vya Dola, Vyama, Jumuia, Raia mmoja mmoja au makundi yeyote ya watu.
MUWAZA inapenda kukumbusha tena kwamba raia wana haki ya kukusanyika kwa njia ya amani na wana uhuru wa kutoa maoni yao bila ya kutishwa, kama ilivyotajwa katika katiba zote mbili, ile ya WATU WA
ZANZIBAR na ile ya serikali ya Muungano wa Tanzania.
MUWAZA inasisitiza juu ya umuhimu wa kuwepo mdahalo wa kila wakati na maelewano baina ya vikosi vya usalama na raia, na kwamba moja ya jukumu kubwa la vyombo vya usalama ni kuwalinda raia na mali zao pamoja na zile za umma. Halikadhalika, raia pia wanatakiwa kuheshimu sheria za nchi zilizojengeka juu ya katiba.
MUWAZA inawanasihi Wazanzibari wote kujenga na kuushajiisha moyo wa masikilizano na maelewano miongoni mwa watu wote wa Zanzibar, viongozi na vyombo vya usalama, na SOTE tujiepusheni kabisa na moyo wa kukaribisha malumbano na mivutano yenye kupelekea utumiaji wa nguvu isiyokuwa na faida kwetu sote.
Tutambuwe kwamba ZANZIBAR ni yetu SOTE WAZANZIBARI, na hasara yeyote kwa nchi yetu ni hasara ya kila mmoja wetu.
Iishi Zanzibar: Mungu ibariki Zanzibar na Watu wake
K.n.y: Mwenyekiti
Jumuiya ya MUWAZA
Nakala:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Kikwete
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dr. Ali Mohamed Shein
Makamo wa Kwanza wa Rais, Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad
Makamo wa Pili wa Rais, Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho
Waziri wa Mambo ya Ndani – Tanzania, Mh Nchimbi
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Tanzania, Bwana Said Mwema
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Bwana Musa A. Musa
Naibu Katibu Mkuu CCM, Zanzibar, Bwana Vuai Ali Vuai
Naibu Katibu Mkuu CUF, Zanzibar, Mheshimiwa Ismail Jussa Ladhu
Jumuiya ya Muamsho, Zanzibar
Vyombo vya habari, Zanzibar
Vyombo vya habari, Tanganyika
No comments:
Post a Comment