Habari za Punde

Serikali Yaanza Kuchukua hatua - Zawataka Wawekezaji kuagiza meli mpya


Na Othman Khamis Ame

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeziagiza Kampuni na Taasisi za Uwekezaji ndani na nje ya Nchi  kuagiza Meli mpya za usafirishaji wa Abiria na Mizigo zinapotaka kuwekeza katika Sekta hiyo hapa Nchini.

Hata hivyo Meli zitakazoagizwa na wawekezaji na Taasisi hizo endapo imetumika lazima isipindukie matumizi ya miaka 15 tu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati akizungumza na Waziri wa Mamo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Tanzania Mh. Benard Membe aliyefika Zanzibar kufariji kutokana na ajali ya Meli ya M.V Skagit iliyozama Jumanne iliyopita.


Balozi Seif alisema taratibu zitaendelea kuimarishwa ili kuona Muwekezaji anayeagiza vyombo vya Usafiri anawasilisha vielelezo vyake vya chombo husika kwa uhakiki wa Kitaalamu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimueleza Waziri Membe kwamba Viongozi wa juu wa Kitaifa wataandaliwa utaratibu wa kutoa mkono wa pole kwa Familia zilizofiwa na kupoteza Jamaa zao katika ajali hiyo.

Aliwaomba Waanchi waliofiwa na kupotelewa na Jamaa zao katika ajali hiyo kuwaorodhesha kwa masheha wao, Wakuu wa Wilaya au vituo vya Polisi kwa uratibu wa baadae.

Mapema Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe amefarajika na hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia vikosi vya Ulinzi vya pande zote mbili katika kukabiliana na maafa yaliyotokea.

Mh. Membe alieleza kwamba hatua hiyo itamsaidia kujibu hoja na maswali  ya Kimataifa  atakayoulizwa kutokana na janga hilo kutokana na nafasi yake kikazi.
Mapema mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kupokea mkono wa pole kutoka kwa Viongozi wa Taasisi mbali mbali za ndani na nje ya Nchi Kufuatia ajali ya meli iliyosababisha vifo vya watu kadhaa.

Balozi Seif alipokea mkono wa pole kutoka kwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Pencheni wa Serikali za Mitaa { NLPF } Ndugu Andru Kuyeyama wenye Makao Makuu yake Mjini Dodoma.

Nd. Andru alimueleza balozi Seif kwamba Wanachama wa Mfuko huo wanaungana pamoja na wenzao kutokana na msiba huu ulioigusa Jamii yote Nchini.

Balozi Seif pia alipokea mkono wa pole kutoka kwa Uongozi wa Kampuni ya Prime Time Promotion inayoendesha Redio ya Coconut F.M.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo Ndugu Ali Khatib Dai alimueleza Balozi Seif kwamba ajali hiyo imeigubika jamii katika msiba mzito.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi alisema kwa sasa Serikali inajaribu kuangalia njia ya kudhibiti wa vyombo chakavu kwa kuzipitia upya sheria zilizopo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Mkurugenzi anayeshughulikia Masuala ya Afrika na Carribean wa Umoja wa Ulaya { EU } Bibi Fransisca Mosca.

Mazungumzo hayo yamefanyika hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif aliuomba Umoja huo wa Ulaya EU kuangalia uwezekano wa kusaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kutafuta mbinu za upatikanaji wa Usafiri wa uhakika kati ya Visiwa vya Zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuwa na Meli zake kama kawaida baada ya zile zilizokuwa zikitumika kupitwa na muda wake wa matumizi.

Naye Mkurugenzi huyo anayeshughulikia masuala ya Afrika na Carribean Bibi Fransisca Mosca alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kwamba Ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Umoja huo na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla utadumishwa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.