Na Othman Khamis, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi
Seif Ali Iddi, amewatahadharisha waumini wa dini ya kiislamu, wenye tabia
kuitafsiri kur-ani kwa manufaa yao binafsi.
Alisema tabia hiyo ni mbaya na yenye
kumchukiza Mwenyezi Mungu na kwamba wakati umefika kwa waislamu kuachana nayo
tabia hiyo mara moja.
Balozi Seif alieleza hayo katika viwanja vya
Chuo cha Kiislamu cha Al-Haramain jijini Dar es Salaam, kwenye kilele cha
maadhimisho ya mashindano ya kuhifadhi kur-ani.
Balozi Seif aliutaka umma wa kiislamu
kuhakikisha unaondosha mifarakano na kuwa wamoja katika kutekeleza maamuru ya
Mwenyezi Mungu.
Balozi Seif Ali Iddi aliitaka jamii ya
kiislamu kuhakikisha inawarithisha kwa kuwahifadhisha watoto wao kitabu
kitukufu cha kur-ani, kwani ndio msingi utakaolijenga Taifa lenye watu wenye
maadili.
Alisema endapo jamii ya kiislamu itajikita
katika kuwarithisha na kuwahifadhisha kur-ani, Taifa litakuwa na vijana
walioshiba kimaadili hali ambayo italisaidia Taifa kuepukana na matatizo mbali
mbali yaliyopo hivi sasa.
Alisema kusoma na kuhifadhi kur-an ni wajibu
wa kila muislamu ili ipatikane faida
ambayo imekusanya mahitaji ya viumbe vyote hapa duniani.
“Ndani ya kitabu hichi kuna mahitaji yetu
yote ya kilimwengu na kesho akhera. Tutapataje mahitaji yetu yote bila ya
kuifahamu kur-ani?”. Alihoji Balozi
Seif.
Akizungumzia suala la mwezi mtukufu wa Ramadhani,
Balozi Seif aliwaasa waumini wenye tabia ya kuswali kila ifikapo mwezi huo kuacha
tabia hiyo inayokwenda kinyume na maamrisho ya dini.
Alisema si vyema kwa waumini kuchagua mwezi
wa kufanya ibada kwani muumini anawajibika kusimamisha swala kila siku katika
kipindi chote cha siku 365 za mwaka mzima pamoja na kufanya mambo yote ya
kheri.
Balozi Seif aliipongeza kamati ya maandalizi
ya mashindano hayo pamoja na wafadhili wote kwa juhudi za kufanikisha jambo
hilo la kheri litakalowajengea hatma njema ya baadaye.
Awali akisoma risala Mwenyekiti wa kamati ya
wanawake wa kiislamu Tanzania, Ukti Shamim Khan alisema lengo la mashindano
hayo ni kuwatia moyo vijana kuipenda kur-ani ambayo itawasaidia kuongoka kwa
kuelekea kwenye ucha Mungu.
Ukti Shamim alielezea masikitiko yake kuona
walimu wanaowaandaa Vijana hao kwa muda mrefu sasa wanasahauliwa, ambapo
alisema kuwa kazi hiyo nzito kinyume na kuangaliwa kama walimu wengine wa skuli
za kawaida zinazotoa elimu ya dunia.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo
Kaimu Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Ali Muhidini, alisema kur-ani lazima
ifanywe kuwa dira katika maisha ya kila siku ya muumini.
Sheikh Muhidini alisema ukosefu wa vijana
wengi kutoelekezwa katika elimu ya dini kumesababisha utitiri wa watoto wa
mitaani unaosababishwa na ukosefu wa malezi bora.
Katika mashindano hayo zawadi mbali mbali
zilitolewa ikiwa pamoja na Laptop Printer, televisheni, misahafu na fedha kwa
washindi waliofungua akaunti ya Amana katika Benki ya Watu wa Zanzibar.
Mashindano hayo yamefadhiliwa na Benki ya
Watu wa Zanzibar, Amana Benki pamoja na Rehema Foundatin inayofadhili wanafunzi
katika vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment