Habari za Punde

Mwanne aja na ‘Midume Mashauzi’


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWIMBAJI wa muziki wa taarab, Mwanne Othman Sekuru, ambaye anatamba katika kibao cha ‘Vifuu Tundu’ alichoshirikishwa na AT, anatarajia kuipua kigomgo chengine baada ya sikukuu ya Idd El Fitr.

Akizungumza mjini Dar es Salaam leo, Mwanne ametaja jina la wimbo huo kuwa ni ‘Midume Mashauzi, na kuwataka mashabiki wake wakae mkao wa kula raha, akisema wimbo huo umeshiba madongo, yanayoweza kumgusa mtu yeyote mwenye tabia hizo.

"Wimbo huo umetungwa na Mohammed Omari Mkwinda ‘Meddy’, na akaniletea, nami nikaweka maneno ya kutia nakshi", alisema Mwanne ambaye ni lulu iliyotupwa na kikundi cha Zanzibar One cha mjini Unguja.

Aliyataja baadhi ya maneno hayo kuwa ni 'Watashindana, lakini watashindwa wenyewe', 'Huna thamani kama mkia wa mbuzi', hufuniki wala hufukuzi nzi’.

Mbali ya kuwa mwimbaji katika kundi la Jahazi Modern Taarab, Mwanne pia ni mtangazaji wa kipindi cha ‘Tamtam za Mwambao’ kinachorushwa katika kituo cha redio ya East Africa ‘EATV’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.