Habari za Punde

ZFA: 'Business as usual' sasa basi. 18 m/- zaingia, wabadhirifu kutoonewa haya

Na Salum Vuai, Maelezo
HALI ya kifedha katika Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imeripotiwa kuanza kuimarika, katika hatua zinazochukuliwa na chama hicho kuwajibika, na kuondokana na ufanyaji kazi wa kimazoea.

Taarifa zilizopatikana baada ya mkutano wa kamati tendaji ya chama hicho uliofanyika juzi katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, zimefahamisha kuwa, ikiwa inakaribia miezi miwili tangu ZFA ipate Rais mpya, tayari shilingi milioni 17 na laki nane, zimeingia katika akaunti ya chama hicho iliyoko Unguja.

Rais wa chama hicho Amani Ibrahim Makungu, amesema shilingi milioni kumi kati ya hizo, ni kamisheni iliyotolewa na Bank ABC, iliyodhamini mashindano ya Super 8, iliyomalizika juzi, ambayo ilishirikisha klabu nane za Tanzania, nne katika Zanzibar na nne za
 Tanzania Bara.

Aidha, alisema shilingi laki nane, ni makusanyo yatokanayo na malipo mbalimbali ikiwemo ada za usajili na mengineyo.

Makungu aliwahakikishia wapenda soka wa Zanzibar kwamba, ZFA ya sasa chini ya uongozi wake, imedhamiria kufanya mageuzi ya kweli yatakayoleta maendeleo ya mchezo huo Unguja na Pemba, ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha na kuzitunza vyema ili zitumike kwa manufaa ya soka la Zanzibar.

Hata hivyo, alisema pale itakapobainika wapo viongozi au watendaji wasiokuwa waaminifu, chama chake hakitakuwa na kigugumizi katika kuchukua maamuzi magumu kwa faida ya ZFA na soka la visiwa hivi.

"Napenda niwatoe wasiwasi wadau wa mpira wa miguu hapa Zanzibar, kwa kuwaambia kuwa uongozi wangu hautakuwa na mzaha juu ya masuala ya fedha, nia ikibainika wapo wanaofanya ujanja ili kujinufaisha, kamati tendaji haitasita kumuwajibisha", alifafanua Rais huyo aliyechukua nafasi ya Ali Ferej ambaye alijiuzulu.


Katika hatua nyengine, Makungu alisema ZFA inakusudia kuajiri katibu muhtasi mwenye sifa, atakayeweza kufanya kazi zote za kiofisi, pamoja na muhasibu mwenye taaluma na akliyebbea kwa ajili ya kuifanya jamii iwe na imani kwa utendaji wa chama hicho.

Alifahamisha kuwa, nafasi hizo zitatangazwa katika siku chache zijazo, kutoa nafasi kwa watu watakaopenda, kuomba kazi hizo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.