Na Mwandishi Wetu
MPAMBANO mkali wa muziki wa dansi, unatarajiwa kushuhudiwa leo katika ukumbi wa Gymkhana, ukizikutanisha bendi pinzani za Dar es Salaam, Msondo Music Band na Ochestra Mlimani Park, wana Sikinde.
Mahasimu hao wakongwe nchini, jana walioneshana umwamba katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni, jijini Dar es Salaam kuanzia saa nane mchana mpaka usiku, katika kusherehekea sikukuu ya Idd El Fitr, kabla kubadilisha jukwaa na kuja hapa Zanzibar.
Pambano hilo la jana, liliandaliwa na Keen Arts, ambapo takriban mwezi mmoja uliopita, bendi hizo zilikuwa zikijiandaa kwa kila moja kujichimbia sehemu yake maalum kwa ajili ya kufanya mazoezi.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mchuano huo wa leo, litakuwa la aina yake hasa kuwa bendi zote zimekamilika.
Kama ilivyokuwa katika onesho la jana jijini Dar es Salaam, hilo litakuwa pambano la kwanza kwa bendi hizo pinzani kupambana siku ya sikukuu ya Iddi katika visiwa vya marashi ya karafuu, tangu zianzishwe, mwaka 1964 Msondo, na mwaka 1978, Sikinde.
Baada ya kutoa burudani kwa mashabiki wao wa manispaa ya mji wa Zanzibar na vitongoji vyake, bendi hizo kesho zitakuwa Kiwemngwa Wilaya ya Kaskazni B, ambako zitaendelea kuwashiana moto katika kijiji hicho cha fukwe za ukanda wa utalii.
Kabla kupanfa jukwaani jana, Msondo ilitokea Dodoma ilikokuwa imeweka kambi, huku Sikinde ikitokea mafichoni kusikojulikana.
Sikinde itakuwa ikiwategemea wanamuziki wake mahiri Hassan Rehani Bitchuka na Ally Jamwaka, waliowasili hivi karibuni wakitokea nchini Marekani, pamoja na Hassan Kunyata, Abdallah Hemba, Habib Jeff, Yusuph Benard na wengineo wengi.
Msondo itawakilishwa na Muhidini Maalim 'Gurumo', Said Mabera, Hassan Moshi, Shaaban Dede, Eddo Sanga, Abdul Ridhiwani na kadhalika.
Mwaka jana bendi hizo zilipambana vikali kwenye ukumbi wa TCC Club sikukuu ya Krismasi ambapo mbali na muziki safi na vituko vya hapa pale zilitoka sare.
No comments:
Post a Comment