Na Mwajuma Juma
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimesema hakifanyi maamuzi yake kwa misingi ya ubaguzi dhidi ya viongozi au wajumbe wa kamati tendaji ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa chama hicho Amani Ibrahim Makungu, amesema hatua ya kumsimamisha Katibu Mkuu Kassim Haji Salum, haikuchukuliwa kwa hisia za kibaguzi, bali imefuata taratibu baada ya kubainika makosa mazito aliyofanya.
Alisema yanayotokea ndani ya chama kwa sasa, ni uthibitisho kuwa kimedhamiria kubadilika na kuendesha mambo kwa mujibu wa katiba na kanuni kuwa ZFA hivi sasa imekubali kubadilika kwa nia ya kuondoa ubababishaji.
Makungu amelazimika kutoa ufafanuzi huo, kufuatia kupokelewa kwa hisia tafauti hatua ya kumsimamisha Kassim, ambapo baadhi ya wadau wanapinga, huku wengine wakiunga mkono.
“Naelewa kila mmoja ana mawazo yake juu ya hili, lakini napenda niwaambie kuwa ZFA hii ninayoongoza mimi, haikuja kuwabagua watu, bali imekuja kufanya kazi ya kuendeleza soka na, na katika hilo, lazima tujisafishe ili kuwapa imani Wazanzibari”, alifahamisha Makungu.
Alisisitiza kuwa, yote hayo yanafanywa kwa dhamira njema ya kuendeleza mpira wa miguu, na kwamba yeyote atakayebainika na madhambi atapaswa kuwajibika, hata akiwa Rais, kwani hakuna aliye juu ya sheria.
“Napenda pia niwafahamishe wale wote wanaosema nimekalia kiti hichi kwa ajili ya kuwabagua wengine, hapana, sio hivyo, ninafanya kazi kwa kuzingatia katiba na maamuzi yote yanapitishwa na vikao halali”, alizidi kuweka wazi.
Kwa hivyo, alisema katika safari ya kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho, hawatamvumilia mtu yeyote atakayekwenda kinyume na katiba na kanuni, iwe kwa kuzipinda sheria za kuendesha soka, au kuhusika na ubadhirifu wa mali za chama.
Alifahamisha kuwa, awali alishindwa kufanya kazi zake kikamilifu, kutokana chama hicho kugubikwa na ‘madudu’ mengi lakini sasa amepata nguvu na kusisitiza kuwa, wanaojifahamu ni wahalifu waliojificha ndani ya chama, ama wajirekebishe au wakubali kuwajibishwa.
Aliwaomba wadau wa soka wa Zanzibar wasisikilize maneno ya wasiopenda mabadiliko katika ZFA, ambayo kwa sasa imejipiga kifua kuwaletea maendeleo wapenda soka wa Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment