Habari za Punde

Wakaguzi waagizwa kuongeza juhudi na kuwa waadilifu

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ,Dk.Ali Mohammed Shein amesema kuwa taasisi zinazohusika na ukusanyaji, ukaguzi na udhibiti wa mapato ya Serikali kuongeza juhudi na uadilifu katika kuitumikia nchi yao .

Akiyasema hayo leo huko Maisara akiwa katika ufunguzi wa Jengo jipya la Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar .

Alisema kuwa wafanyakazi wote wa Serikali waliokabidhiwa dhamana ya kupanga na kutumia fedha za Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa.

Aidha alisema kuwa taasisi zote za serikali yakiwemo makampuni ya umma, taasisi za fedha na mashirika ya umma,kushirikiana ipasavyo na ofisi za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.

Pia kuweza kuhakikisha vitabu kumbukumbu na hati nyenginezo zote zinazohusiana na hesabu za aina zote zinawasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa wakati uliopangwa na unaostahiki kama sheria zilivyoelekeza .

Akieleza kuwa kufanya hivyo kutarahisisha kazi za kudhibiti na kukagua fedha na rasilimali za umma kwa ufanisi wa hali ya juu na kuweza kwenda sambamba na sheria.

Sambamba na hayo Dk Shein aliwataka wafanyakazi hao kulitunza na kulienzi jengo hilo pamoja na mitambo, iliyomo ili kuweza kufikia malengo yaliowekwa na kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Hata hivyo alisema kuwa umuhimu wa kuwa na mipango imara ya serikali na taasisi zote za serikali na za binafsi za kuweza kuwajengea uwezo wafanyakazi wao kwa kuwaandalia mafunzo yanayolingana na sehemu wanazozifanyia kazi kwa lengo la kuzidisha ufanisi .

DK Shein alisema kuwa serikali itaendelea kuimarisha mashirikiano na ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ya Zanzibar kwa kuhakikisha wafanyakazi wanapata maslahi yanayolingana na ugumu wa kazi zao za kudhibiti na kukagua fedha za rasilimali ya umma .

Nae Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Fatma Mohammed Said amesema kuwa ofisi yake imemaliza mpango mkakati wa miaka mitatu yenye malengo mbali mbali ikiwemo kujenga ofisi za kisasa pamoja na kuimarisha mazingira na wafanyakazi wake .

Jumla ya shilling millioni 328.4 zilitumika kwa kujengea jengo hilo kuweka mitambo mbali mbali ya Mawasiliano pamoja na kuweka vitendea kazi vya kisasa ambavyo vinavyokwenda na wakati .Jengo jipya la Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni la pili kufunguliwa la mwanzo lilizinduliwa miaka miwili iliopita ,jengo hili limejengwa na kampuni ya Stars construction .

Aidha mdhibiti huyo alisema kuwa juhudi kubwa ya Serikali imewezesha kukamilisha jengo hilo katika kupanga na kutekeleza mipango madhubuti ya maendeleo nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.