Habari za Punde

Nyumba yengine yateketea kwa moto Chake chake Pemba

 
Wananchi mbali mbali wa vitongoji vya mji wa Chcke chake, wakiangalia moto uliokuwa ukiounguza nyumba ya Riziki Hamad Ali, huko Madungu chake chake jana ambapo nyumba hiyo iliteketea yote pamoja na vitu vyote vilivyokuwemo ndani.(picha na Haji Nassor, Pemba)





Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kikiwa katika harakati za kuzima moto uliotokea jana kwenye nyumba ya Riziki Hamad Ali huko Madungu Wilaya ya Chake chake Kisiwani Pemba, ambapo katika nyumba hiyo kuliteketea kila kila kitu na hadi sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana (picha na Haji Nassor, Pemba)
 
Na Haji Nassor, Pemba
IKIWA majanga ya kuungua nyumba moto yakiendelea kutikisa Kisiwa cha Pemba, jana tena kumetokezea moto mkubwa na kuunguza nyumba yote na vitu vilivyokuwemo ndani ya nyumba hiyo huko Madungu Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba
 
Kadhia hiyo ilioanzia siku mbili kabla, kwa kuunguza kanga na begi kwenye nyumba za jirani na kutoonekana kwa chanzo, jana ulianza majira ya saa 2:10 asubuhi, wakati mwenye nyumba hiyo Riziki Hamad Ali akiwa anakwenda kazini.
 Moto huo ulifanikiwa kudhibitiwa vyema na Kikosi cha Zima Moto na Uokozi, kwa kushirikiana na vikosi vyengine, ikiwa ni Jeshi la Polis na wananchi waliokuwa karibu na eneo hilo.

 Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuudhibiti moto huo, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Uokozi Mkoa wa Kusini Pemba, Ame Ali Khamis alisema kuwa mara baada ya kupokea taarifa hiyo walifika mapema kuzima moto huo.
 Alisema kuwa wamefanikiwa kutokana na kuwa na vifaa kamili vya kuzimia moto ambapo pia kutokana na mioundombinu iliopo katika nyumba hiyo.
 Kamanda Ame,alieleza kuwa hadi sasa hawajaelewa chanzo cha moto huo mkubwa ambao ulikuwa ulionekana mithili ya imani za kishirikiana kutokana kuwaka na kuzima kimaajabu.
 ‘’Kwa kweli sisi KZU mara baada ya kupata taarifa hii tulikuja mbio na kuanza kuzima, lakini kwa hili niwapongeza sana wenzetu wa Jeshi la Polisi na wananchi kwa kuonyesha ushirikiano wao kwetu’’,alieleza Kamanda huyo.
 Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Hassan Nassir alisema kuwa wamepokea taarifa hiyo wakiwa ofisini na vijana wake walifika mapema katika eneo na kushirikiana na wakoaji.
 Alifafanua kuwa, hadi sasa hawajajua chanzo cha moto huo, lakini Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi ili kutambua chanzo.
 
‘’Bado hatujaelewa chanzo cha moto huo mkubwa na sisi kama Jeshi la Polisi tutafanya upelelezi wa haraka, lakini tunawapongeza KZU kwa kudhibiti moto huo’’,alifafanua Kamanda huyo.
 
Mapema mmiliki wa nyumba hiyo Riziki Hamad Ali (26), alisema kuwa aliondoka nyumbani kwake na kwenda kazini ambapo kabla hajafika alipata taarifa ya kuungua nyumba yake moto.
 
Akieleza kwa masikikitiko alisema kuwa hakukua na kitu chochote cha matumizi ya ueme kilichokuwa wazi na ameshangaa kupokea taarifa hiyo muda mfupi tu tokea kuondoka.
 
Kwa kweli hadi sasa sijaelewa chanzo cha moto huo maana nilipoondoka mimi kwenda kazini, vitu vyote vimezimwa na wala vyengine havitumiki kabisa ’’,alieleza.
 
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa awali waliona moto mkubwa kutoka katika nyumba hiyo  ambayo ilikuwa imekomewa na kupiga kelele na wakaanza kuzima.
 
Walieleza kuwa baada ya kuona hivyo baadhi yao waliwapigia Kikosi cha Zimamoto na Uokozi na ghafla walifika na kuanza kuuzima licha vitu vyote kuungua.
 
Taarifa zilizopatikana katika eneo hilo zilieleza kuwa siku mbili kabla ya kutokezea hayo, nyumba ya ndugu yake Riziki, Ali Hamad kuliungua kanga moto na hapakuwa na chanzo jambo ambalo liliwashangaaza waliokuwemo ndani ya nyumba hiyo.
 
Tukio jengine la maajabu lilitokezea kwenye nyumba hiyo hiyo ya Ali, mara hii kukiungua nguo zilizokuwemo kwenye beki ambapo beki lilibaki salama na nguo zote kuteketea.
 
Hii inaifanya kuwa nyumba ya 14 kukumbwa na ajali ya kuungua moto katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja Kisiwani Pemba, ambapo baadhi ya wananchi wanahusisha moto huo na iamani za kishirikina.
 
Wiki iliopita jumla ya nyumba 13 ziliungua moto kwa siku tofauti huko Tumbe Kaliwa Mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa maajabu kutokana na kuunguza baadhi ya vitu na vyengine kubaki salama.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.