Habari za Punde

Kamati ya Taifa Sherehe na Mapambo yakutana kujadili maandalizi ya sherehe za mapinduzi

 
Na Othman Khamis Ame
Kikao cha Kamati ya Taifa ya Sherehe na Mapambo Zanzibar kimekutana chini ya Menyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuendelea kujadili maandalizi ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kutimia miaka 49.
Wajumbe wa Kikao hicho kutoka Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali pamoja na Vikosi vya Ulinzi wamefanya mkutano wao katika Ukumbi wa Jumba la Wananchi { Peoples Palace } liliopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Kikao hicho kilijadili Mada tofauti ikiwemo Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Majengo na Taasisi za Umma, uzinduzi wa Miradi mipya ya Jamii, pamoja na Maandalizi ya gwaride la maadhimisho ya sherehe hizo zinazotarajiwa kufikia kilele chake Januari 12 Mwakani.

Akitoa Taarifa ya baadhi ya mapitio ya Kikao kilichopita Katibu wa Kamati ya Taifa ya Sherehe na Mapambo Zanzibar ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohd alisema maagizo yaliyotolewa katika Kikao kilichopita yametekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Sekta ya Elimu inatarajiwa kuchukuwa asilimia kubwa ya Miradi itakayohusishwa kwenye maadhimisho ya Sherehe zijazo za Mapinduzi ya Zanzibar.
Akikiahirisha Kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sherehe na Mapambo Balozi Seif Ali Iddi ameelezea matumaini yake kutokana na mabadiliko ya ufanisi wa maandalizi ya Sherehe hizo.
Wajumbe wa Kikao hicho wanatarajiwa kukutana tena kwa maandalizi ya mwisho ya sherehe hizo mnamo Tarehe 11 Disemba mwaka huu siku moja kabla ya kuanza kwa zoezi la pamoja la gwaride la Vikosi vya ulinzi na usalama kwa ajili ya sherehe hizo zitakazofikia kilele chake katika Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekutana na Mfanya Biashara wa Kimataifa wa Kampuni inayomiliki Viwanda vya Samaki kutoka Nchini Uturuki Bwana Ahmed Uzur mazungumzo ambayo yalifanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika Mazungumzo hayo Bwana Ahemd Uzur amesema amevutiwa na mazingira mazuri yaliyopo hapa Zanzibar na tayari ameshaonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyake hapa Zanzibar.
Bwana Ahmed alimueleza Balozi Seif Kwamba Kampuni yake mbali ya kuzalisha Samaki, Mafuta ya Samaki lakini pia ina uwezo wa kuzalisha Umeme kwa kutumia upepo.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Zanzibar bado inakaribisha wawekezaji wa Nchi za nje kuwekeza Vitega uchumi vyao hapa Nchini kwa lengo la kukidhi mahitaji yake ya kutoa huduma kwa Jamii.
Balozi Seif alimshauri Mfanya biashara huyo kutoka Nchini Uturuki kuandaa Mipango yake itakayoweza kutoa sura halisi ya namna anavyoweza kuwekeza hapa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.