Na-Mwanaisha Muhammed-Maelezo Zanzibar
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dkt Omar Makame Shauri amesema kila mtu ana wajibu wa kujilinda asiambukizwe na Ukimwi sambamba na kuwalinda wengine wasiambukizwe na Ugonjwa huo.
Amesema njia pekee ya kutimiza hilo ni kuchukua tahadhari ya kujikinga na Ukimwi kwa kuzingatia kwamba Ugonjwa huo unaweza kumpata mtu yeyote bila kujali Jinsia hadhi au Umri alionao.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo huko Ofisini kwake Shangani mjini Zanzibar alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Disemba 1.
Amesema wanajamii wanawajibu wa kubadili tabia za hatari walizonazo ambazo kama watazikumbatia ni sawa na kujitia kitanzi katika maisha yao.
Amezitaja baadhi ya tabia hizo kuwa ni pamoja na kuwa na wapenzi wengi kwa wakati mmoja, kufanya ngono zisizo salama,kutokuwa waaminifu katika ndoa na kutumia sindano zisizosafishwa.
Akizungumzia suala la unyanyapaa nchini kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Dkt. Omar amesema umepungua kwa kiasi fulani lakini bado unaendelezwa kufanywa katika jamii jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa Mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Dkt Omar amekemea vikali tabia ya unyanyapaa na kusema kuwa kuwepo kwa unyanyapaa hupunguza ufanisi katika juhudi za kupambana na Ukimwi kwani anayenyanyapaliwa anaweza kuwaambukiza wengine kwa makusudi.
Ameisihi jamii kuwachukulia watu waliopata Maambukizi ya Ukimwi kuwa bado ni wanajamii wanofaa kuheshimiwa,kulindwa na kushirikishwa katika maisha ya kila siku.
Akizungumzia kuhusu changamoto zinazoikabili Tume ya Ukimwi amesema kuwa ni pamoja na kutegemea sana fedha za wahisani katika utengenezaji wa Programu za Ukimwi sambamba na Washirika wa Maendeleo kutoa vipaombele vyao vinavyofautiana na vya hapa Zanzibar.
Mkurugenzi alisema katika kukabiliana na hali hiyo Serikali itajitahidi kutafuta mbinu mpya zitakazo saidia kuongeza kiwango cha fedha za ndani kwa ajili ya kuziba pengo ili mapambano dhidi ya Ukimwi yawe yenye tija zaidi na endelevu .
Aidha alifahamisha kwamba maadhimisho hayo kwa mwaka 2012 yanatarajiwa kufanyika Mangapwani Wilaya ya Kaskazini ambapo Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya,Juma Duni Haji.
Kauli mbiu.ya mwaka huu ni wito wa kimataifa unaowataka wanajamii kuchukua juhudi ili yasiwepo maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa kuwataka wanajamii kuchukua hatua za kujikinga na maambukizo mapya.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment