Habari za Punde

Dk Shein akutana na watendaji wizara ya elimu pamoja na wizara ya katiba na sheria


Watendaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, wa idara mbali mbali wakiwa katika Mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, katika utekelezaji wa
Mpango wa kazi za Wizara hiyo,wakiwa katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria, katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar ,(kushoto) Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif,

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar ,(kushoto) Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
 Watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, wa Idara mbali mbali wakiwa katika Mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo,wakiwa katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar
Watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, wa Idara mbali mbali wakiwa katika Mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, katika
utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo,wakiwa katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar
[ Picha na Ramadhan Othman,IKULU.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeeleza kuwa kuhamia kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika kampasi ya Tunguu kumesaidia sana katika kukiwezesha chuo hicho kujipanua na kuwa na mazingira mazuri ya kufanya kazi.
Maelezo hayo yametolewa leo na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee walishiriki.

Akisoma Taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ali Juma Shamuhuna alisema kuwa hata hivyo, idadi ya wanafunzi walioandikishwa kujiunga na chuo hicho imeongezeka kutokana wanafunzi 1,413 hadi wanafunzi 1,837.
Alisema kuwa ongezeko hilo la wanafunzi limetokana na uamuzi wa SUZA kuongeza program mbili mpya za masomo.
Aidha,Uongozi huo ulieleza kuwa iaddi ya wanafunzi wanaosoma katika taasisi za Elimu ya Juu wanaodhaminiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar imeongezeka sana kutoka wanafunzi wapya 209 hadi wanafunzi wapya 800.
Uongozi huo ulieleza kuwa ongezeko hilo limetokana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar kutoka TShs. Bilioni 4 hadi TShs. 8.
Wizara hiyo pia, ilieleza kuwa ujenzi wa skuli 13 mpya za sekondari kati ya 16 umekamilika ambapo skuli 9 mpya zimeshaanza kuchukua wanafunzi na wakati huo huo ujenzi wa skuli tano mpya za sekondari za ghorofa unaendelea katika maeneo ya Mpendae, KiembeSamaki na Kwamtipura, Mkoa wa Mjini Magharibi, Kibuteni kwa upande wa Mkoa wa Kusini Unguja na Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba.
Wizara ilieleza kuwa, awamu ya kwanza ya ujenzi wa kampasi ya Chuo cha Ualimu cha Benjamin William Mkapa huko Mchanga Mdogo, Pemba umekamilika na ujenzi wa awamu ya pili unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka 2013.
Wakieleza baadhi ya changamoto zinazoikabili Wizara hiyo, ilieleza kuwa uhaba wa nafasi za kusomea hasa katika ngazi ya elimu ya msingi imesababisha baadhi ya skuli na madarasa kuwa na wanafunzi wengi kwa darasa hasa skuli za Wilaya ya Magharibi.
Katika kupunguza uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na Hisabati sekondari, Wizara, imepokea walimu 13 wa masomo hayo kutoka Nigeria, pia, imeshafanya mazungumzo na ubalozi mdogo wa Misri, India na Ghana ili kupatiwa waalimu.
Changamoto nyengine iliyoelezwa na Wizara hiyo ni kuwepo kwa walimu wengi wa kike kupendelea kufundisha katika Mkoa wa Mjini Magharibi kutokana na kufuata waume zao hali ambayo imesababisha uwiano usio sawa wa mgawanyo wa waalimu.
Tatizo la wanafunzi wengi kutojitokeza kwa hiari kulipa fedha walizokopa katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, mpaka wafuatiliwe na wengine wanashindwa kurejesha mikopo kutokana na kukosa ajira nalo limejitokeza..
Dk. Shein pia, alikutana na Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Waziri wake Mhe. Abubakar Khamis na kueleza utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.
Wizara hiyo ilieleza kuwa suala la upatikanaji wa haki limetekelezwa kupitia njia mbali mbali ikiwemo matengenezo ya majengo ya Mahakama Kuu Vuga, Mahakama ya Kadhi Mwanakwerekwe na Mahakama ya ChakeChake kwa upande wa Pemba ili kuweka mazingira mazuri ya kuendesha kesi katika ngazi mbali mbali.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria imeendelea kuimarishwa kwa kupatiwa watendaji na vitendea kazi pamoja na mafunzo ya uandishi wa sheria ambapo pia, Wizara imefanikiwa kutayarisha na kukamilisha Mpango Mkakati wake kwa utekelezaji wa kipindi cha miaka mitano 2011/2016.
Sambamba na hayo, Wizara hiyo ilieleza kuwa afisi yake ya Pemba imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba majukumu yote ya Wizara, ikiwemo kulinda na kusimamia haki za wananchi, yanatekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha.
Nae, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kuzipongeza Wizara hizo sambamba na kuzitaka kuendeleza juhudi na mikakati yake iliyojiwekea ili kuweza kupata mafanikio zaidi.

1 comment:

  1. Waziri wangu shamuhuna ananiangusha sana, kama utatembelea katika maskuli muandishi, utaona hali mbaya hasa katika skuli za sekondanri za wilaya ya mjini magharibi,nenda katemblee skuli ya darajani,hamamni,forodhani,Vuga kule, na skuli nyengine, hazina ukarabati wowote, skuli hazipigwi rangi, kuta zimechoka zimejaa mashimo, hata sakafu vile vile.

    Nilisikitishwa sana kuona skuli ziko katika hali hiyo, pia wizara ya elimu ya zanzibar inaniangusha katika suala la walimu, walimu wetu hasa ambao wanao fundisha wanafunzi kuanzia form 3 mpaka 6 hawana viwango , wale wanafunzi wali fail form4 ndio wanasomea uwalimu na baadae walimu hao eti kufundisha wanafunzi wa form6.

    Hapo kwa kweli ni mfumo mbaya ambao unaangusha kiwango cha elimu yetu kwa upande wa zanzibar halafu tunasingizia wabara wanatuonea wanatufelishia wanafunzi wetu au watoto wetu.

    Tunahitaji walimu wenye kiwango cha degree kufundisha wanafunzi wa secondary ili tuweze kupiga hatua na elimu yetu kuwa bora zaidi.

    shickland

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.