Habari za Punde

Kila la kheri Zanzibar Heroes




Leo jioni timu ya Taifa ya Zanzibar – Zanzibar heroes itajitupa uwanjani kuvaana na timu ya taifa ya Kenya – Harambee Stars katika mchezo wa nusu fainali kugombea kombe la Cecafa katika uwanja wa Mandela mjini Kampala Uganda.

Zanzibar Heroes iliweza kufikia nusu fainali baada ya kuitoa timu ya taifa ya Burundi kwa mikwaju ya penelti baada ya mcezo kumalizika bila ya kufungana.

Kibarua cha leo ni kigumu sana ukizingatia timu ya Taifa ya Kenya ni mojawapo katika timu nzuri zilizoonesha kandanda la kuvutia na pia Kocha wa Kenya ameongeza timu yake baada ya kuwaita wachezaji wawili aliowaacha nyumbani kutokana na utovu wa nidhamu.


Ingawa Zanzibar Heroes haina rekodi nzuri dhidi ya Harambee stars kwani katika mara 11 zilizowahi kukutana katika mashindano haya Kenya imeshinda mara saba, kutoka sare mara tatu na imefungwa mara moja tu. Hata hivyo kinachoshindaniwa hapa si rekodi bali uimara wa timu tuliyo nayo

Heroes hata hivyo wapo katika hali nzuri kisaikolojia kwa kuweza kuziondoa timu kubwa zenye majina hivyo Harambee Stars itajikuta ina wakati mgumu jioni ya leo kwani ari ya ushindi kwa vijana wetu imezidi kuongezeka licha ya timu hii kupata maandalizi dhaifu na hafifu ambapo walikosa mechi za maana za kujipima nguvu kabla ya mashindano haya.

Hata hivyo soka walilolionesha, kujiamini kwa wachezaji wetu huku kila mmoja akijua nini wajibu wake akiwa uwanjani, kusikiliza ushauri wa kocha Salum Bausi, ni vitu muhimu vilivyoisaidia timu yetu kufanya vizuri na kufika nusu fainali.

Nahodha wa Zanzibar Heroes Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema ‘ Haoni timu nyengine itakayowasumbua baada ya kuiondoa Burundi kwenye robo fainali’.
Kiungo Suleiman Kassim 'Selembe' ndiye anaonekana kuwatia khofu wakenya kwani ndiyo injini ya timu ya Zanzibar hivyo wanatarajia kumkaba ilivyo.

Katika michezo ya nusu fainali mwaka huu mashindano ya Cecafa yamebakiwa na timu nne ambazo ni waasisi wa mashindano haya mwaka 1947 nao ni Kenya, Tanganyika, Uganda na Zanzibar.

Blog ya ZanziNews inaitakia kila la heri Zanzibar heroes leo hii na ituletee raha kwa kuwaondoa wakenya na kusubiri mchezo wa fainali ambao tuna imani ya kulirudisha kombe la Cecafa kama tulivyofanya mwaka 1995.

Come on Heroes

2 comments:

  1. Afadhali 'Cholo' amerudi asidie kuimarisha ukuta kule nyuma!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.