Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Malik Abdulla Juma akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi eneo la Paa la Jengo la Wataalamu na Madaktari Bingwa wa Cuba liliopo mkabala na Bustani ya Victoria Mmazi Mmoja ambalo linahitaji kufanyiwa matengenezo.
Kulia yao ni baadhi ya Madaktari hao wakiongozwa na Mkuu wa Chuo cha mafunzo ya Udaktari wa Afya kinachosimamiwa na Wataalamu wa Cuba Dr. Rebeca Lahera Cambara
Balozi Seif alifanya ziara hiyo fupi kwa lengo la kuangalia mazingira wanayoishi wataalamu hao na namna ya kutafuta mbinu za kuyaimarisha zaidi ili kuleta utulivu kwa wakaazi hao.
Na Othman Khamis Ame OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itajitahidi kuwajengea mazingira bora ya makaazi Wataalamu wa Sekta ya Afya wanaopangiwa kutoa huduma za kijamii kwa Wananchi hapa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Balozi Seif alisema hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua makaazi ya Madaktari na Wataalamu wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba kwenye Jengo wanaloishi liliopo pembezoni mwa Bustani ya Victoria Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.
Balozi Seif amesema hitilafu ndogo ndogo zilizojitokeza katika Makazi ya Wataalamu hao zitatafutiwa ufumbuzi wa haraka ili kutoa fursa kwa Tataalamu hao kufanya kazi zao kwa utulivu.
Aliuagiza Uongozi wa Wizara ya afya kufanya Tathmini ya haraka ya makisio ya matengezo hayo ili kuwahi kujikinga na msimu wa masika unaotarajiwa kuanza miezi michache ijayo.
“ Tunawajibika kuwajengea mazingira mazuri wataalamu na madaktati wetu ili wawe na uwezo wa kufanya kazi zao za kutoa huduma kwa utulivu”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Madaktari na Wataalamu hao wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba kwa jitihada zao za kuendelea kutoa huduma za Afya kwa imani na upendo.
Alisema utaratibu huo wa muda mrefu unaendelea kujenga uhusiano wa Kihistoria uliopo mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kati ya Zanzibar na Jamuhuri ya Watu wa Cuba.
Mapema Mkuu wa Chuo cha mafunzo ya Udaktari wa Afya kinachosimamiwa na Wataalamu wa Cuba Dr. Rebeca Lahera Cambara ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wanaoupata katika kutekeleza vyema majukumu yao.
Hata hivyo Dr. Rebeca alisema yapo matatizo madogo madogo yaliyojitokeza katika Makazi yao ya upungufu wa huduma za maji safi kwa nyumba yao ya Mombasa na paa kwa ile iliyopo Bustani ya Victoria Mnazi Mmoja.
Jumla ya Madaktari na Mabingwa wa Afya kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba wapatao 17 wanatoa huduma za Afya Zanzibar ambao 11 kati yhao wapo Kisiwa cha Unguja na Madaktari 6 wapo Kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment