Habari za Punde

Waandishi waaswa kufichua maovu wanayofanyiwa wenye ulemavu wa akili

Na Ali Issa Maelezo Zanzibar 11/12/2012
Katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dk. Omar Dadi Shajak, amewaomba waandishi wa habari kufichua maovu ya udhalilishaji wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa akili ili kuondoa vitendo vya unyanyasaji vinavyowakabili watu hao.
Hayo ameyasema leo huko EACROTANAL mjini Zanzibar wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari juu ya namna ya kuandika na kuripoti taarifa za watu wenye ulemavu wa akili ambao wanaendelea kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji na hujuma mbaya.


Amesema watu wenye ulemavu wa akili ni sawa na watu wengine na wanastahiki kupewa haki zao za msingi katika jamii ili wajijue thamani yao kwa taifa.
Amesema hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la udhalilishaji wa watu hao kwa kuwabaka na kuwafanyia vitendo vyengine vya unyanyasaji jambo ambalo si zuri kuachiwa.
“Kuna baadhi ya wazee huishia mezani kimazungumzo baada ya watoto wao kubakwa. Kisheria haipasi kufanya hivyo na lazima watu wanaojihusisha na unyama huo wafichuliwe”, alisema Dk Shajak.
Aidha alifahamisha kuwa, baadhi ya waandishi wa habari huwaandika vibaya watu wenye ulemavu wa akili pale wanapofanya mambo yao wakiwa faragha, na kusema jambo hilo ni kosa kubwa na lazima faragha ya kila mtu iheshimiwe.
Katibu huyo aliwasisitiza waandishi hao kuandika ukweli na kufuatilia kwa makini habari za walemavu wa akili vijijini kwa kuwafichua wale wanaowadhalilisha ili wakomeshwe na iwe fundisho kwa wengine.
Aidha aliwaomba wahariri kuanzisha vipindi katika majukwaa ya habari kwa lengo la kuelimisha umma namna ya kukaa na watu hao, kuwapenda na kuwatunza kwani kila mmoja anaweza kuwa mlemavu madhali bado anaishi.
Nae mkufunzi kutoka chuo cha sheria Tunguu ambae pia ni mwandishi wa habari Ali Uki, alisema kuwa walemavu ni sehemu ya jamii na wana haki sawa na wengine, na kwamba kumuhudumia mlemavu ni suala la lazima na sio fadhila.
“Jamii isiwadharau watu hawa kwani na walemavu wapo dunia nzima huu ni mtihani kwetu , Haki zao zi heshimiwe na itikadi isipewe nafasi”, alisema Uki.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.