Na Haji Nassor, Pemba
ZAIDI ya shilingi 120 milioni, zinahitajika kwa ajili ya
kumalizia ujenzi wa jengo maalum la kufanyia mitihani la ghorofa moja na vyumba
vitano vya madarasa katika skuli ya sekondari ya Uweleni Mkoani Pemba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwalimu
anaeshughulikia majenzi skulini hapo, Mohamed Ussi Shaame alisema kwa sasa
wameshatumia shilingi 22 milioni, kwa ajili ya msingi.
Alisema kati fedha hizo walizotumia, shilingi 3.5 milioni
ambapo ilikuwa ni saruji paketi 200, walipewa msaada na Benki ya Watu wa
Zanzibar (PBZ), miezi michache iliopita.
Ussi alieleza, fedha nyengine walizotumia hadi kufikia
hatua hiyo ya msingi, ni shilingi milioni 2, kwa hatua ya wali kutoka mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo na baadae shilingi 8 milioni.
Aidha alisema, hata Mwalikishi wa jimbo la Mkoani, Abdalla
Mohamed Ali, amechangia shilingi 500,000 katika ujenzi huo unaoendelea skulini
hapo.
Mwalimu huyo anaesimamia majenzi, alifahamisha kuwa, fedha
zote hizo hawakukabidhiwa taslimu, bali ni vifaa mbali mbali kama vile kokoto,
mawe, nondo na mchanga.
Hata hivyo, alisema waalimu, wazazi na wanafunzi, nao
hawako nyuma katika kuendeleza ujenzi wa jengo hilo, ambalo ni agizo la Wizara
ya Elimu la kila skuli kuwa na kumbi maalum za kufanyia mitihani.
Alifafanua, kila mwalimu kwa hiari yake kila mwisho wa
mwezi wamewakua wakichangia shilingi 1,500 pamoja na michango ya miradi midogo
midogo ya skuli.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Shehe Hassan aliwaomba wale wote waliosoma
skulini hapo, kuaona umuhimu wa
kuchangia ujenzi huo, ili umalizike kwa wakati.
Akizungumzia mikakati ya kuzipata fedha hizo wanazozihitaji,Mwalimu
huyo alisema ni pamoja na kusaka wafadhili wa nje.
Mkakati mwengine, ni kuwatafuta wafadhili wa ndani ikiwa ni
pamoja na Wabunge, Wawakilishi na wafanyabiashara wenye nia kusaidia pamoja na
kufikisha kilio chao serikali kuu.
No comments:
Post a Comment