Na Radhia Abdalla, Pemba
JUMLA ya wanafunzi 104 wa Chuo cha Ufundi Kengeja Wilaya ya
Mkoani Pemba,hulazimika kulala katika nyumba za walimu,msikitini na madarasani
kufuatia uhaba wa mabweni unaokikabili
chuo hicho.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi chuoni hapo, Kaimu
Mwalimu Mkuu wa chuo hicho, Rashid Ali
Said alisema ni wanafunzi 56 tu pekee, ndio wanaolala kwenye mabweni chuoni hapo.
Alisema chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 160, ambao kati yao,ni wanafunzi 56 wa kike ndio
wanaolala kwenye bweni wakati waliobakia wakiendelea kulala katika mazingira
yasiyo rasmi.
Alifahamisha kuwa hali hiyo inatokana na uhaba mkubwa wa
mabweni jambo ambalo huwakosesha utulivu wa masomo hususani kwa wanafunzi wa
kiume.
“Kwa kweli uhaba wa mabweni katika chuo hichi ni changamoto
kubwa, ambayo inatukabili na inahitaji kutatuliwa haraka,’’ alieleza Kaimu
Mwalimu Mkuu huyo.
Akizungumzia kuhusu uhaba wa walimu pamoja na vifaa vya
kufundishia, tatizo hilo ni kubwa na kwa
kiasi kikubwa linachangia kuanguka kwa ufaulu wa masomo kwa wanafunzi.
Alisema chuo hicho ni kimojawapo ambacho kinaingiza wanafunzi wenye vipaji maalum,
lakini imeonekana vipaji vya wanafunzi hao hudumaa kutokana na
ukosefu wa vifaa vya kufundishia na walimu.
Alisema suala la walimu ni muhimu katika chuo hicho ambacho
ndio chachu ya maendeleo ya taifa kwani
kuna mafunzo ya aina mbali mbali yanayotolewa ikiwa ni pamoja na ufundi.
Alisema kukosekana kwa waalimu wa kutosha ni miongoni mwa
changamoto kubwa inayopelekea wanafunzi
kutofanya vizuri katika mitihani yao ya taifa, hasa miaka ya hivi
karibuni tofauti na mwanzoni mwa
kuanzishwa kwa chuo hicho.
Aliwataja walimu wa masomo hasa ya ufundi ndio ambao kwa
sasa wamekuwa tatizo kubwa jambo ambalo linatishia matokeo mabaya kwa
wanafunzi.
Mwanafunzi Mariam Salim wa (kidato cha sita) chuoni hapo
ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia vifaa vya ufundi ili
kukabiliana na changamoto iliyopo.
Chuo cha ufundi Kengeja ni miongoni mwa vyuo vikongwe hapa
Zanzibar ambacho kwa muda mrefu sasa kinaendelea kukabiliwa na changamoto
kadhaa ikiwa ni pamoja na uhaba wa walimu, vitendea kazi na uhaba wa mabweni.
No comments:
Post a Comment