Habari za Punde

Prof. Rai ataka uhusiano wa kielimu Zanzibar, Uturuki uimarishwe

Na Asya Hassan
 
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Profesa Idris Rai amesema mahusiano baina ya Zanzibar na Uturuki yaliyoanza tokea karne ya 18 yanapaswa kuimarishwa zaidi ili kuweza kukuza taaluma kati ya nchi hizo mbili.
 
Prof. Rai alieleza hayo jana katika mkutano wa 8 wa kimataifa wa taasisi ya Elimu na Utafiti ya vyuo vikuu vya Uturuki (ACTR-ADAM), uliofanyika chuo kikuu cha taifa cha Zanzibar, Vuga. Mkutano huo ulitathmini uhusiano uliopita, wa sasa na uhusiano wa baadae kati ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Uturuki.
 
Alisema kuimarika kwa uhusiano huo ni chachu ya kuweza kukuza uchumi na elimu kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na kuweza kupata wasomi bora ambao wataweza kuiletea maendeleo nchi.


Aidha alifahamisha kuwa Zanzibar na Uturuki zina uhusiano mkubwa kutokana na nchi hizo kufanana katika utamaduni wake. Prof. Rai alisema kuendelezwa mashirikiano ya pande mbili kutaweza kuisadia Zanzibar kubuni nyanja mpya ya kukuza elimu kwa wananchi wake.
 
Akizungumzia maendeleo ya chuo hicho, alisema SUZA kimepiga hatua kubwa katika kufundisha kada mbali mbali ikiwemo udaktari (PhD) katika masomo ya Kiswahili.
 
Hata hivyo, alisema chuo hicho kinatarajia kuanzisha kada mpya za utalii, afya, mawasiliano, kompyuta na kilimo.
 
Nae Rais wa ADAM Prof. Mehmet Bulut alisema ili kuweza kukuza taaluma ya elimu Zanzibar ni vyema kuwepo mashirikiano ya wataalamu wa pande zote mbili katika kukuza elimu.
 
Katika mkutano huo mada mbali mbali zilijadiliwa, ikiwemo athari za utalii wa kimagharibi kwa uchumi, mila na utamaduni wa Zanzibar, iliyowasilishwa na Dk. Issa Ziddy Haji.
 
Mada nyengine ni tatizo la chakula kwa nchi zinazoendelea hasa ukanda wa Afrika Mashariki, iliyowasilishwa na Dk. Sabri Er.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.