Na
Hafsa Golo
MWANAFUNZI
Ruwaida Mohmoud Ramsa anaesoma skuli ya
Mtoni ameibuka mwanafunzi bora kitaifa katika mitihani ya kidato cha pili
iliyofanyika Novemba mwaka uliopita.
Ruwaida
amechaguliwa kuwa mwanafunzi bora kati ya wanafunzi 19,676 waliofanya mitihani
hiyo.
Nafasi
ya pili imechukuliwa na mvulana Saleh Abdalla Juma kutoka skuli ya
Mwanakwerekwe ‘B’ huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na mvulana
mwengine, Khalid Muhidini Haji kutoka skuli ya Mwembemakumbi.
Kwa
upande wa mitihani ya darasa la saba, mwanafunzi bora kitaifa ni Abdulsalami
Juma Khamis kutoka skuli ya Mtopepo ‘A’, akifuatiwa na Said Mkubwa Salum kutoka
skuli ya Kiembesamaki na nafasi ya tatu kitaifa ikichukuliwa tena na mvulana,
Abdulrazak Machano Hassan kutoka skuli ya Mtopepo B.
Akitangaza
matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna
alisema wanafunzi 12 wote wa kidato cha pili wamefutiwa matokeo baada ya
kubainika kufanya udanganyifu, ambapo ni upungufu wa kesi 5 ikilinganishwa na
mwaka 2011 ambapo waliofutiwa matokeo walikuwa 17.
Alisema
kati ya wanafunzi waliofanya udanganyifu, wanane wanatoka skuli ya Donge.
Wengine
ni kutoka skuli ya Regeza Mwendo (3) na Mwembeladu mwanafunzi mmoja.
Kwa
upande wa watahiniwa wa kidato cha pili, wanafunzi 11,195 wamechaguliwa kujiunga
kidatu cha tatu katika skuli mbali mbali, kati yao wasichana ni 6,768 na
wavulana 4,427, ambapo ni sawa na asilimia 56.9 ya watahiniwa wote.
Katika
ngazi hiyo kulikuwa na watahiniwa 19,679 kati yao wasichana 11,045 na wavulana
8,644.
Takwimu
hizo zinaonesha wanafunzi 8,484
wameshindwa kabisa kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.
Aidha
wanafunzi walioandikishwa kufanya mitihani ya kidato cha pili walikuwa 21,019
lakini waliofanya mitihani hiyo walikuwa 19,679 hivyo wanafunzi 1,340 hawakufanya
mitihani hiyo kutokana na sababu mbali mbali ambazo hata hivyo hazikutajwa.
Shamuhuna
alisema kiwango cha ufaulu kwa mitihani ya kidato cha pili kimeongezeka kwa
asilimia 0.8 ikilinganishwa na mwaka 2011.
Alizitaja
skuli za Bwefum, Umbuji, Uzi,Ubago,Pongwe Pwani, Michamvi na Mtende, kwa Unguja
kuwa ndio skuli zilizofanya vibaya zaidi kwa kupasisha wanafunzi kidogo na
kwamba madarasa yao yatafungwa.
Kwa
Pemba alizitaja skuli tatu za tiro kuwa ni Kisiwa Panza, Makoongwe na Ndagoni
ambazo zimepasisha wanafunzi wanane, saba na sita na hivyo madarasa yao pia
yatafungwa.
Kwa
upande wa watahiwa wa darasa la saba,
wanafunzi 17,511 wamefaulu kujiunga na kidato cha kwanza , kati yao
wasichana 9652 na wavulana 7859 sawa na asilimia 76, ambapo kuna upungufu wa
asilimia 5.2 ikilinganishwa na mwaka 2011.
Aidha alisema wanafunzi wa darasa la saba waliopata
asilimia 60 hadi 100 ni 1,501.
Wanafunzi walioandikishwa kufanya mitihani hiyo walikuwa
24,940 ambapo wasichana 12,960 na wavulana 11,980.
Waziri huyo alisema waliofanya mitihani ni 23,039 ambapo
wanafunzi 1901 hawakufanya mitihani hiyo kutokana na sababu mbali mbali.
No comments:
Post a Comment