Katibu Mkuu Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto Bibi Fatma Gharib Bilal akimpatia taarifa Balozi Seif kuhusu matengenezo makubwa na majengo ya wazee Sebleni mara ya kuzindua rasmi majengo hayo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi funguo ya chumba chake Mzee Daudi Seif mara baada ya kuizindua rasmi nyumba ya wazee hao iliyofanyiwa matengenezo makubwa hapo Sebleni Mjini Zanzibar
Bibi Tiba Vuai akionekana mwenye furaha akipokea ufunguo wa chumba chake kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika hafla ya uzinduzi wa jengo lao lililofanyiwa matengenezo makubwa
Balozi Seif akifanya mzaha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa umma na Utawala bora Mh. Haji omar Kheif.
Kati kati yao ni Waziri wa Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar na Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Mh. Salmin Awadh Salmin.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe haitakuwa na mjadala katika jukumu lake la kuendelea kuwatunza wazee wasiojiweza wanaosihi katika makazi yao waliyotayarishiwa mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua majengo yaliyofanyia matengenezo makubwa pamoja na miundo mbinu katika makaazi ya wazee yaliyopo Sebleni Mjini Zanzibar.
Alisema suala la ujenzi wa makaazi ya wazee wasiojiweza ni moja kati ya ahadi zilizotolewa na Chana cha Afro Shirazy Party mara baada ya Mapinduzi na serikali ya Mapainduzi ya Zanzibar inaandaa sera Maalum ya kuweka taratibu ya kuwatunza wazee kisheria .
“ Utaratibu wa kuendelea kuwatunza wazee upo kama kawaida kwani tunaelewa kwamba Jamii isiyo na utaratibu huo inaeleweka kwamba imepotoka kabisa”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa mashirika ya Kitaifa na Kimataifa zikiwemo Taasisi Binafsi kushirikiana na Serikali katika kuwatunza wazee na kutoa rai kwa wanafunzi wa vyuo Vikuu na Sekondari kutenga siku maalum ya kujumuika na wazee katika harakati zao za usafi wa mazingira.
Naye Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohd alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwaondoshea aibu iliyokuwa ikiwapata wazee wanaonyanyasika kutokana na ukosefu wa makaazi.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Fatma Gharib Bilal alisema ujenzi wa majengo hayo yaliyojumuisha nyumba moja, ukumbi wa Mikutano, sambamba na miundo mbinu ya umeme na maji umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 429,900,000/-
Matengenezo hayo yamekuja kufuatia kuungua kwa moto nyumba hiyo ya wazee usiku wa terehe 6/1/2011 ,ukosefu wa uzio uliosabisha wizi wa vitu vyao na ubovu wa miundo mbinu ya maji na umeme.
No comments:
Post a Comment