Habari za Punde

Jamii yatakiwa ibadilike katika matumizi ya chakula


Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Chakula na Lishe Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa kwanza wa Baraza hilo uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean view Migombani Mjini Zanzibar.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Taifa la Chakula na lishe wakiwa katika Mkutano wao wa kwanza wa baraza hilo uliofanyika Zanzibar Ocean View Migombani Mjini Zanzibar

Mtaalamu wa Kilimo Bibi Mastura Kassim akitoa mada ya mfumo wa utekelezaji wa masuala ya uhakika wa chakula na lishe kwenye mkutano wa kwanza wa Baraza la Taifa la uhakika wa chakula na lishe hapo Zanzibar Ocean View Migombani Mjini Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu waPili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohd Aboud Mohd akichangia mada katika mkutano wa kwanza wa Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe hapo Zanzibar Ocean View Migombani.Kushoto ya Mh. Aboud ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundo mbinu Mh. Issa Haji Ussi na kulia ni Waziri wa Kilimo Mh. Suleiman Othman Nyanga.


Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Mh. Dadi Faki Dadi akichangia mada katika mkutano wa kwanza wa Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe Zanzibar hapo Zanzibar Ocean View Migombani.
Kushoto ya Mh. Dadi ni Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakar na Kushoto ya Mh. Dadi ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pembe Juma Khamis.
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Wakati umefika kwa Jamii Nchini kuanza kubadilika kwa haraka katika matumizi bora ya chakula kwa lengo la kuziwezesha familia zao kujenga afya bora inayokubalika kitaalamu.
Hayo yameelezwa kwenye Mkutano wa kwanza wa Baraza la uhakika wa chakula na lishe uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Migombani Mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wakitoa mada katika Mkutano huo Wataalamu wa Sekta ya Kilimo Bwana Ali Ramadhan, Bwana Mzee Rajab na Bibi Mastura Kassim walisema tabia ya watu kupenda matumizi makubwa ya mchele mbali ya kupoteza fedha nyingi za kigeni kwa uagizaji wa bidhaa hiyo lakini pia yanaukosesha mwili kupata virutubisho vinavyohitajika.

Walisema ili uhakika wa chakula upatikane nguvu za uzalishaji wa mazao mbali mbali zinahitajika kwa lengo la kuondokana na utegemezi wa chakula kimoja tu cha mchele.
“ Asilimia 41% ya chakula kinachotumika Nchini huagizwa nje ya Zanzibar. Mfano bidhaa ya mchele Zanzibar huzalisha Tani 13,000 wakati uagizaji bidhaa hiyo nje ya nchi hufikia Tani 46,000 mwaka 2007 na Tani 50,000 kwa mwaka 2011”. Alifafanua Bwana Ali Ramadhan.
Hata hivyo Bwana Ali Ranadhan alielezea kwamba zao la Muhogo kwa sasa ndio pekee linalofikia hatua ya kutosheleza mahitaji ya ndani wakati zao la mpunga ambalo ndio chakula kikuu nchini linaendelea kuwa la kubahatisha.
Bwana Mzee Rajab kwa upande wake alisema udumavu wa watoto hapa Zanzibar unaonekana kupanda kutoka Asilimia 11% hadi Asilimia 30%.
Alisema udumavu huu wa watoto ambao huanzia tumboni mwa mama unatokana na wananachi wengi hapa Zanzibar kubadilisha mfumo wa matumizi ya chakula ambao umejikita zaidi katika vyakula vya mafuta.
Mapema akiufungua Mkutano huo wa kwanza wa Baraza la Taifa la uhakika wa chakujla na lisheZanzibar, Mwenyekiti wa Baraza hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uwajibikaji, mshikamano pamoja na uratibu wa uhakika ndio mambo ya msingi yatakayoliwezesha Taifa kuwa na uhakika wa chakula.
Balozi Seif alisema jukumu la Taifa kuwa na uhakika wa chakula si la Wizara ya Kilimo pekee bali kila Taasisi, ambapo uzoroteshaji wa kazi kwa Taasisi moja unaweza kusababisha utekelezaji mbovu wa mambo yaliyopangwa.
Alifahamisha kwamba Taifa lisilokuwa na uhakika wa chakula na lishe usalama wake unakuwa mashakani jambo ambalo wananchi wanaweza kupoteza utu wao na hili si vyema kwa Wajumbe wa Baraza hilo wakaliachia kuendelea ndani ya dhamana yao.
“ Zanzibar yenye uhakika wa chakula na lishe inawezekana iwapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake”. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Baraza la Taifa ya Uhakika wa Chakula na Lishe Zanzibar Balozi Seif.
Balozi Seif alielezea faraja yake kuona kwamba mada zilizojadiliwa katika Baraza hilo zimeelezea hali ya uhakika wa chakula na lishe Nchini ambayo sio nzuri jambo ambalo ni changamoto zinazolikabili Taifa ambazo Baraza hilo halinabudi kujipanga vizuri katika kukabiliana nayo.
Alisema Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe Nchini linawajibika kusimamia utakelezaji wa Sera ya uhakika wa chakula na lishe hapa Nchini kwani ndio chombo cha mwisho cha kufanya maamuzi katika kutekeleza masuala yoyote ya uhakika wa chakula na lishe.
“ Majukumu tuliyopewa na Taifa letu ambayo imani yangu kila Mjumbe anayafahamu ni makubwa mno na ili tufanikiwe vizuri kuyatekeleza majukumu hayo tunahitaji kuwajibika,kushikamana pamoja na kuwa na uratibu wa uhakika”. Alifafanua Balozi Seif.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.