Na Bashir Nkoromo
PAMOJA
na mambo mengine Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kuzitumia sherehe za miaka
36 ya kuzaliwa kwake, kufanya tathmini ya uchaguzi wake mkuu wa viongozi
mbalimbali uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana.
Lengo
la tathmini hiyo ni kujifunza au kukumbushana kwa kina changamoto
zilizojitokeza, hivyo kuitumia fursa hiyo kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya
uchaguzi mkuu mwingine wa ndani ya Chama wa mwaka 2017.
Hayo
yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ndogo ya makao
makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam.
Nape
alisema, sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa CCM zitafikia kilele chake Februari 3,
2013, na zitafanyika kitaifa kwenye uwanja wa Lake
Tanganyika mjini Kigoma.
Alisema,
mgeni rasmi katika sherehe hizo ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na
zitahudhuriwa pia na Makamu Wenyeviti wa CCM (Zanzibar) Rais wa Zanzibar, Dk.
Ali Mohamed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na wajumbe
wote wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa wakiongozwa na Katibu Mkuu,
Abdulrahman Kinana.
"Baadhi
ya viongozi hasa sekretarieti na maofisa wa chama tutaenda Kigoma kwa kreni, na
chama kimeamua kutumia usafiri huu kama sehemu ya kupongeza juhudi zinazofanywa
na serikali katika kuboresha huduma za usafiri huo," alisema Nape.
Nape
alisema, uamuzi wa kufanya kilele cha sherehe hizo Februari 3, 2013 ni kutokana
na tarehe yenyewe ya kuzaliwa kwa CCM, ambayo ni Februari 5, 2013 kuwa siku ya
kazi, hivyo kutoweza kutoa fursa kwa wanachama kushiriki kwa ufanisi katika
sherehe hizo muhimu kwao.
"Sherehe
hizi za miaka 36 ya kuzaliwa CCM zinafanyika ikiwa ni takriban miezi miwili tu
tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa ndani ya chama na jumuiya zake zote
ukamilike Novemba 13, 2012, kwa hiyo ni sherehe muafaka kujipongeza na vilevile
kuwashukuru wanachama wake kwa kukamilisha kwa ufanisi uchaguzi huo,"
alisema Nape.
Alisema
ili kuwashirikisha wanachama katika ngazi zote, uzinduzi wa sherehe hizo
utafanyika kwenye matawi yote, Jumatano Januari 30, , kwa kufanya mikutano ya
wanachama wote, nafasi ambayo itatumika kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa
CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 katika ngazi hizo.
Alisema
Alhamisi Januari 31 itakuwa ni siku ya Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo wanachama
wa jumuiya hiyo watashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ambazo
alisema ni pamoja na usafi wa mazingira na upandaji wa miti.
Alisema
Februari 1 itakuwa Siku ya Umoja wa Wazazi ambapo watashiriki katika shughuli
za kijamii ikiwa ni pamoja na kupanda miti, kushiriki katika ujenzi wa miradi
ya maendeleo kama vile madarasa, zahanati, nyumba za walimu na kadhalika.
Shughuli
nyingine itakayofanywa na wazazi ni kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na
jumuiya zake wa mwaka 2012, na pia watajadili mafanikio ya jumuiya hiyo yenyewe
kwa miaka 36 iliyopita. Jumamosi Februari 2 itakuwa siku ya Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT).
Nape
aliendelea kueleza kwamba shughuli zitakazofanywa na wanachama hao wa UWT ni
kufanya usafi, kupanda miti, kutembelea na kufariji wagonjwa katika hospitali
na vituo vya afya, kutembelea vikundi vya uzalishaji mali vya kina mama,
kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 na
mwisho ni kujadili mafanikio ya UWT kwa miaka 36 iliyopita.
Siku
ya kilele cha sherehe hizo ambazo alisema kaulimbiu yake ni Umoja ni Ushindi
kutafanyika matembezi ya mshikamano na kwamba wanachama wa CCM na jumuiya zake
zote nchini kote ambazo ni UVCCM, Wazazi na UWT watafanya matembezi ya
mshikamano katika kila tawi kwa muda ambao kila tawi litaona unafaa kwa
kuzingatia hali halisi ya mazingira ya eneo husika.
Vilevile
itafanyika mikutano ya wanachama wote kwenye matawi, kata, wilaya na mikoa
ambayo itatumika kupokea na kujadili maazimio ya mkutano mkuu wa CCM
uliofanyika tarehe 11 – 13 Novemba, 2012 na utekelezaji wa mradi wa awamu ya tatu
wa kuimarisha chama.
No comments:
Post a Comment