Habari za Punde

…Mkurugenzi Manispaa aondolewa madarakani


Na Mwantanga Ame
SAKATA la kuwepo kwa mikataba tete ndani ya Baraza la Manispaa, serikali imemuondoa madarakani Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa huku ikimpa uhamisho aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa baraza hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha utekelezaji mapendekezo ya kamati teule ya Baraza la Wawakilishi iliyoundwa kuchunguzaa utendaji wa baraza la manispaa. 

Hapo awali wajumbe wa baraza hilo waliikataa ripoti hiyo kwa madai kuwa serikali imeshindwa kuonesha wazi hatua inazokusudia kuzichukua kwa wahusika waliotajwa ndani ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo ilitolewa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi baada ya kuomba kuundwa kamati teule ya baraza hilo kutokana na kujitokeza mikataba tata ambayo baraza la Manispaa iliingia na wafanyabiashara.


Matokeo ya ripoti hiyo yalimtaja aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Rashid Ali Juma kuwa ni muhusika mkuu wa mikataba hiyo kwa kushirikiana na Mhasibu Mkuu wa baraza hilo.

Dk. Mwinyihaji akielezea hatua ambazo serikali imezichukua juu ya suala hilo ni kumuondoa madarakani Mkurugenzi kwa barua yenye kumbukumbu BLM/40A/C.9/VOLIX/160 ya tarehe 22/10/2012.

Barua nyengine ambayo waziri huyo aliitaja ilikuwa inamuhusu Mkurugenzi huyo yenye kumbukumbu namba OR/TMV/R.10/C.4/VOLXII/61 ya tarehe 30/12/2012.

Mhasibu wa baraza hilo pia alipewa barua namba OR/IKL/U.40/VOL.IV/180 ya tarehe  14  Januari 2013.

Alisema Wizara hiyo imeanza kuwachukulia hatua watu hao huku wengine wakiwaacha kufanyiwa kazi na ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

Alisema katika kulifanyia kazi hilo pia serikali inakusudia kuipitia upya mikataba yote ya baraza hilo.

Alisema taratibu za mikataba ya serikali ilihitajika wakati wa kuifunga kuishirikisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali lakini hilo halikufanyika kwa mikataba ambayo baraza hilo.

Alisema uimarishaji wa baraza hilo utaenda sambamba na mabadiliko ya kanuni mbali mbali ambapo baada ya kukamilika kwake ndipo wataweza kuona ni hatua zipi waweze kuchukua kwa watu wanaodai kulidai braza hilo.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walipinga tena na maelezo hayo ya serikali lakini baada ya Spika Pandu Ameir Kificho kuyatolea maelezo wajumbe hao walikubaliana nayo na kuipitisha ripoti hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.